Monday, 23 September 2013

Hivi ni kwanini wanawake hawapendani na Kulikoni wakunga kuwanyanyasa wajawazito?

 
Na kibaya zaidi ni kinamama ndiyo wanaowafanyia ufirauni wanawake wenzao pamoja na ukweli kwamba wanapaswa kuheshimu taaluma yao katika utoaji wa huduma.
Kabla sijaeleza baadhi ya shuhuda za kinamama walionyanyaswa na wanawake wenzao, niulize swali moja rahisi lakini lililojaa mashaka makubwa. Hivi ni kwanini wanawake hawapendani?
Swali hili nakumbuka liliwahi kuulizwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwanzoni mwa miaka ya 1980 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) pale Arusha, akishangaa hata pale kinamama wanapogombea nafasi mbalimbali za uongozi walikuwa hawapigani tafu ili washinde, na badala yake wanachagua zaidi wanaume.
Na kikubwa zaidi kilichokuwa kinasababisha hali hiyo kutokea ni wivu eti akichaguliwa fulani ataringa,mara yule anajidai sana hapaswi kuwa kiongozi, mara yule ni masikini hafai na vijisababu vingi visivyo na msingi wowote.
Kumbe hawa wanaowasema kuwa hawafai pengine ndiyo haswa wenye ari na moyo wa kuongoza na kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hiyo ilikuwa ni upande wa uongozi. Lakini upo upande mwingine wa huduma ambao nimeona leo nizungumzie hasa pale kazi yenyewe inakuwa ya wito na maadili yake yakiwa wazi, lakini bado wanataaluma husika wanawafanyia wenzao vituko.
Sekta ya afya ni miongoni mwa sekta nyeti katika nchi yoyote ile na ndiyo maana hata bajeti yake kidogo huwa iko juu. Na hiyo inatokana na ukweli kwamba sekta hiyo inashughulikia afya na uhai wa binadamu.
Lipo eneo moja muhimu ambalo ndilo naligusia hapa, fani ya uuguzi na ukunga. Eneo hili linasimamiwa na wanawake, pia wanaume. Mara nyingi upande wa wanaume, utoaji wa huduma umekuwa mzuri, lugha ya upole na wasikivu kwa wagonjwa tofauti na wanawake.
Hii naongelea wanataaluma hawa wanapowahudumia wagonjwa wanawake.
Nijikite katika eneo la wakunga katika wodi za kujifungulia wanawake. Kwanza ipo mifano mingi ambapo wanawake ambao wanakwenda hospitali wanapofikia muda wa kujifungua hupata misukosuko mingi hasa suluba toka kwa wauguzi au wakunga wanaopaswa kuwasaidia.
Wapo kinamama watatu ambao nimezungumza nao hivi majuzi wakisimulia vituko walivyokumbana navyo wakati wamepata uchungu kwa ajili ya kujifungua katika hospitali za Dar es Salaam. Yafuatayo ndiyo malalamiko yako.
“Mimi nilipatwa uchungu majira ya saa nane mchana, mbio nikaenda katika hospitali ambako nilikuwa nafanyia kliniki. Ajabu ni kwamba mkunga niliyemkuta, nikamweleza tatizo langu, alinitizama na kuniambia…kwani una mimba wewe? Nenda zako nyumbani muda bado.
“Nilishangaa sana kwani tayari namsikia kabisa mtoto anataka kutoka. Nikiwa nimekaa kwenye benchi, akapita muuguzi mwingine nikamuita nikamuomba anisaidie uchungu umechachamaa najisikia kujifungua. Huyu akanichukua hadi kwenye chumba cha leba.
Akamuita na muuguzi mwingine(siyo yule aliyeniambia niende nyumbani.
“Wakaanza kunihudumia na muda mtoto akatoka. Kidogo yule muuguzi aliyeniambia sina mimba akatokea akataka naye kushiriki kunihudumia, nikamwambia hapana awaache tu hawa wengine kwani hakuonyesha nia ya kunisaidia tokea mwanzo. Mungu mkubwa nikajifungua salama.”
Mwingine anasema; “Nilifika hospitalini uchungu ukiwa bado haujashika kasi. Nikapewa kitanda nikalala hadi kesho yake. Akaja muuguzi mmoja akanitizama na kuanza kuniambia; “wewe sitaki ukae kabisa hapo kitandani kwa sababu sitaki kukuona hapa. Nataka ujifungue uende zako.
Nikawa nashangaa kwanini mimi niambiwe hivyo wakati tuko kinamama wengi vitanda sita? Kisha akaniamuru nitoke nje nikatembee. Nilitembea kuzunguka maeneo ya hospitali karibu siku nzima, huku miguu imenivimba.
Matokeo yake nilichoka sana hata ule usiku ambao nilipelekwa leba siku weza kula. Ilipofika asubuhi nikawa nimechoka na hata mapigo ya mtoto hayasikiki. Ikabidi wakanitundikia dripu ya maji ya chakula kuniongezea nguvu na kisha dripu mbili za uchungu. Mungu mkubwa nikajifungua salama kwani kule leba nilipata wauguzi na wakunga wazuri. Lakini wodini yule muuguzi alinichukia sana bila sababu. Ila nimemsamehe bure.
Mama mwingine yeye alijifungua pia salama lakini kule leba alikutana na timu ya wakunga jeuri.
Anasema; “ walinipa maneno makali huku wakidai eti nimewasumbua sikuwa nasikiliza yale wanayoniambia nifanye ili nijifungue salama.
“Hata hivyo baada ya kujifungua ilibidi niwaombe msamaha kwani ilikuwa ni mimba ya kwanza na sikuwa na uzoefu wowote kabla. Ila nilijiuliza; kwanini wasitusaidie kwa kutuliwaza kwa maneno ya faraja ni wanawake wenzetu? Hivi wanawake tunapendana kweli?”
Mpenzi msomaji, bila shaka umewasikia kinamama hao na vitimbwi walivyokumbana navyo wakati wakijiandaa kwenda kujifungua. Utakumbuka pia tuliwahi kuandika kuhusu mama mmoja aliyejifungua akiwa amesimama katika moja ya hospitali za hapa Jijini Dar.
Katika mapokezi anaomba huduma ya haraka lakini wauguzi wakawa nawanamhoji maswali badala ya kumkimbiza kwanza leba, matokeo yake mtoto akafyatuka akiwa amesimama. Mungu mkubwa mtoto hakupatwa na madhara baada ya uchunguzi wa kina.
Haya. Wanawake kwanini hawaoni raha kuwahudumia wanawake wenzao hasa pale wanapokuwa katika wakati mgumu kama vile kujifungua? Swali langu kubwa hapa ni kwamba, kwanini wakunga wawanyayase wajawazito? Hili ni tatizo ambalo yafaa lipimwe kwa macho mawili ili liweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment