Monday, 16 September 2013

Hivi ni kweli mwanzo wa penzi tamu, mwisho wa penzi shubiri?

wanandoa wawili wanaodhamiria kuvunja ndoa zao ili washikamane kama mke na mume. Yaani waachane na wenza wao, kisha waanzishe mahusiano mapya na ikiwezekana kuoana.
Sababu kubwa wakieleza; mmoja kachoshwa na mumewe kumpiga kila mara na kumnyima kufanya shughuli yoyote ila kukaa tu nyumbani. Mwingine mkewe anamkwaza kila kukicha hata kufiakia hatua kutaka wagawane mali, jambo ambalo mume alikubali na kumruhusu achukue kila apendacho kwani yeye(mume) atatafuta vingine.
Wawili hao ambao ndoa zao zinawaka moto, awali kabla ya kuoa au kuolewa walishaonyesha mvuto wa kupendana lakini ukapita upepo utawapeperusha kila mtu upande wake wakajikuta wanapata wenza wengine.
Sasa leo wamekutana na waliposimuliana kuhusu maisha kumbe kila mmoja anayo machungu yake. Ndipo wanajiandaa kukata shauri wajitoe kwenye vifungo vya ndoa, kisha waanzishe maisha mapya. Kwenye makala iliyopita nikauliza “ anayetaka kuacha na anayetaka kuachika wamepania kuoana…je, hili litawezekana?
Mpenzi msomaji, mambo ndiyo mambo. Usione ndoa hizi watu wanasimama madhabahuni au mbele ya sheikh ukadhani unyenyekevu ule kwa wengine unakuwa wa kudumu. Huwa wanavutiana pumzi tu na pale kila mmoja atakapojua madhaifu ya mwenzake ndiyo utamu huanzia hapo. Upo hapo msomaji wangu? Maisha Ndivyo Yalivyo.
Haya ndiyo maoni mbalimbali
Naam. Yupo msomaji anasema hivi; “Mimi naona hawana upendo wa dhati ndani ya ndoa zao, bora wanchane kila mmoja aende kwa anaye mpenda (Ramadhan Abdala wa Same, Gonja).
…Kwa kweli ndoa miaka hii zina matatizo makubwa. Kwa upande wa huyu kijana aliyeachwa na mkewe afanye taratibu za kuachana(talaka). Na mwenzie vile vile(bibie), mbona inawezekana lakini itabidi wahamie kwingine! Maana haitakuwa salama kuwa karibu na wataliki wao(mama Lulu, Kitunda, Dar).
...Mimi naona bora hawa ambao ndoa zao zinafukuta waoane kwa sababu wote wamepata misukosuko ya kutosha.
…Nimefurahika kwa hii makala yako nzuri. Mimi nadhani itakuwa ngumu sana kuliwezesha hili suala mpaka kuwa ndoto ya kweli kwani wote ni wanandoa kama ulivyosema anti.. Isitoshe, mwanamke hajapewa talaka yake na mwanaume pia hajapeana talaka ila wametengana kwa muda. Kwa hilo itakuwa ni vigumu sana kulifanikisha(0766676898).
…Hao hawatawezana kwa sababu mmoja wapo akifanya kosa tu ataambiwa ndio maana mkeo amekuacha kwani wanaume na wanawake wote sawa. (Mie ant Rahma wa Tabata, Dar).
…Naanza kutokana na stori ilivyo ni wazi kwamba hawa walipendana tangia mwanzo ila tu kikwazo hali ya uchumi. Kila mmoja alienda alikoona kuna maslahi. Ila kwa sasa wana historia sawa na bado wanapendana. Wataishi kwa furaha waoane tu(Naitwa Rama).
…Naitwa Laurenti.J.Mainda wa Chalinze. Ninachoona mimi suala la wanandoa hawa kuoana ni gumu kwao kwa sababu wanachokifanya ni sawa na mama mjamzito kuanza kununua nguo za mtoto kabla ya kuzaliwa. Kwa maana nyingine wangebadilisha mawazo hayo na kufikiri namna ya kukabiliana na ndoa zao kwa kushirikisha viongozi wa dini inaweza kuwa ni suluhu kwao.
…Nianze kwa kuchangia mada ; Hawa jamaa wamepania kuoana kila mmoja huko aliko amechoshwa na madhila yake. Mie anti nina mtazamo tofauti.
Nataka niwakumbushe kuwa hata mwanzo wa ndoa zao hakukuwa na matatizo, mambo yamejitokeza baada ya kupita miaka mingi na hata sasa wameanza vizuri hatujui siku zijazo kitatokea nini!
Ni jana tu nilikuwa na rafiki yangu tukijadili kuhusu mke anayemfanyia mume visa akiachika baada ya siku hujikuta anaona haya bora hata asingeachika.
Wakati mwingine anapopata bahati akimpata mume basi hutia akili. Kwa hili la hawa jamaa nina mashaka nalo kwani nakumbuka pana wimbo wa zamani usemao; mwanzo wa mapenzi tamu kama asali, mwisho wa mapenzi chungu kama shubiri.
…Kuacha ndoa zao inawezekana kwani tayari siyo ndoa bali ni ndoano. Cha msingi kila mmoja aache ndoa yake ili waishi kwa amani(Musa H. Kilingo.mazava, Morogoro).
 
 

No comments:

Post a Comment