Friday, 20 September 2013

Jay Dee kupamba Redd`s Miss Tz

Mwanamuziki bora wa mwaka, Judith Wambura 'Lady Jay Dee' ambaye kwa sasa anatamba na vibao vyake vya Yahaya na Joto Hasira, anatarajiwa kutumbuiza katika shindano la urembo la taifa 'Redd's MissTanzania 2013' litakalofanyika keshokutwa kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa Kinywaji cha Redd's, Victoria Kimaro, alisema  mazungumzo na msanii huyo yamekamilika ambapo pia alimtaja msanii mwingine atakayesindikiza onyesho hilo kuwa ni Mganda, Mike Ross.

Kadhalika Victoria alisema shindano hilo litakalofanyika kuanzia saa 1:00 usiku litapambwa na burudani ya wasanii wa ngoma za asili wa Kikundi cha Mama Afrika.

"Kwa kuwa usiku huo ni usiku wa wanawake, tumeona Lady Jay Dee aongoze burudani. Wasanii hawa wanahadhi ya kutumbuiza usiku huo," alisema meneja huyo.

Akimzungumzia msanii huyo wa Uganda, meneja huyo alisema, anatarajiwa kuwasili nchini leo mchana na kesho atashiriki kwenye mazoezi maalumu yatakayoshirikisha wasanii wote pamoja na warembo wanaowania taji hilo la taifa.

Mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga, alisema maandalizi yamekamilika na tiketi kwa ajili ya onyesho hilo, zimeanza kuuzwa jana sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Lundenga alisema watakaonunua mapema tiketi ya VIP za Sh. 100,000 kila moja watauziwa kwa Sh. 80,000 huku akitaja kiingilio cha chini katika shindano hilo kuwa ni Sh. 50,000.

Mratibu huyo pia aliwashukuru wadhamini wote waliojitokeza mwaka huu kwa ajili ya kudhamini shindano hilo likiwemo Gazeti la NIPASHE linalochapishwa na Kampuni ya The Guardian Ltd.

Warembo 30 kutoka sehemu mbalimbali nchini, wanatarajiwa kuwania taji hilo linaloshikiliwa na Brigitte Alfred kutoka Kanda ya Kinondoni jijini ambaye kwa sasa yuko Indonesia akijiandaa kupanda jukwaani kuwania taji la dunia ifikapo Septemba 28, mwaka huu.

Tayari warembo watano ambao ni Severina Lwinga kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam ambaye ni Redd's Miss Personality, Prisca Clement (Redd's Miss Talent), Clara Bayo (Redd's Miss Sports Woman), Happiness Watimanywa (Redd's Miss Photogenic) na Narietha Boniface aliyetwaa Redd's Miss Tanzania Top Model, wote wameshatinga hatua ya 15 bora ya shindano hilo.

Mshindi wa taji hilo mwaka huu atabebeshwa dhamana ya kuiwakilisha nchi katika shindano la urembo la dunia mwakani sambamba na zawadi ya Sh. milioni nane pamoja na gari jipya lenye thamani ya Sh. milioni 15.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment