Friday, 20 September 2013

Kikwete atosa wabeba ‘unga’

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakiwa wamebeba dawa za kulevya (unga) nje ya nchi kwa sababu biashara hizo ni haramu na uvunjaji wa sheria.
Alitoa msimamo huo juzi usiku wakati alipokutana na kuzungumza na Watanzania waishio katika Jimbo la California, Marekani katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, Kikwete alisema Watanzania wamejiingiza kwa kiasi kikubwa katika biashara za ovyo ovyo kama vile dawa za kulevya.
Alionya kuwa serikali yake haitawatetea wanaokamatwa wakishiriki biashara hiyo.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi zetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyo ovyo kiasi hicho.
“Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa, lakini ukifanya biashara ya dawa za kulevya ama kubaka watu hatukutetei kamwe,” alisema.
Kuhusu suala la uraia wa nchi mbili, Rais Kikwete alisema kuwa serikali yake haina uhakika kama litaweza kuwemo katika katiba mpya kwa sababu halimo hata kwenye rasimu ya katiba licha ya kupendekezwa na chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Lakini sisi katika CCM tumelizungumza na kuliweka katika mapendekezo yetu mapya tulipokaa kama Baraza la Katiba. Tunataka lizungumzwe.
“Hatuna hakika kama litawekwa katika rasimu ijayo, lakini tutaendelea kulisemea. Kubwa ni kwamba hili ni jambo ambalo halitapata sauti za kutosha kulisemea,” alisema.
Rais alifafanua kuwa faida za suala hilo zinaeleweka hata kama inaelekea kuwa hakuna watu wengi wanaokereketwa na jambo hilo kiasi cha kulisema vya kutosha katika mjadala wa katiba.
Aliwataka Watanzania wanaoishi nchi za nje kuishi kwa amani, kuheshimu sheria na kutojiingiza katika mambo yanayoweza kuwaingiza katika matatizo.
“Lazima muwe raia wema. Mliamua wenyewe kuja kuishi katika nchi hizi. Nchi hizi zina sheria zake. Kama mtaamua kuwa raia wabaya wanaovunja sheria mtaingia katika matatizo,” alionya.
Kuhusu ombi la Watanzania waishio nje kuruhusiwa kupiga kura, Rais Kikwete alisema kuwa serikali yake haina tatizo wala pingamizi kuhusu suala hilo ili mradi tu Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwe na uwezo wa kulifanikisha.
Katika hatua nyingine, rais amewataka Watanzania kuisemea, kuijenga na kuitetea nchi yao badala ya kushiriki katika kuikejeli na kuidharaulisha.
Alisema kuwa kuisemea na kuitetea Tanzania ni wajibu wa kila Mtanzania, awe anaishi ndani ya nchi ama ughaibuni.
Rais aliongeza kuwa ni jambo la ajabu kuona kazi ya kuisemea, kuitetea na kujenga jina zuri la Tanzania inafanywa zaidi na watu wa nje kuliko baadhi ya Watanzania na hasa wale wanaoishi nje.
Pia Rais Kikwete alisisitiza kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kuwa nchi ya kuomba na kupokea misaada na hisani kama kweli inataka kupiga hatua za haraka za maendeleo.
Kwamba Tanzania imeanzisha utaratibu wa kuteua mabalozi wa heshima katika nchi mbalimbali duniani kama namna ya kujenga na kuendeleza kwa haraka zaidi maslahi yake.
Rais alitoa kauli hiyo baada ya kumsimika rasmi Ahmed Nassoro Issa kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania katika Jimbo la California na kufungua ofisi ya ubalozi katika Mtaa wa Redwood Highway.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment