Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Waziri Ally Chilakwechi, amepigwa na watu wasiojulikana baada ya kumvamia nyumbani kwake eneo la Mchangani mjini Tunduru na kujeruhiwa vibaya.
Sheikh Chilakwechi akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru alikolazwa, alisema alishambuliwa na watu wasiojulikana juzi.
Akielezea mkasa huo, alisema siku ya tukio alifuatwa na watu watatu majira ya saa 2:30 usiku nyumbani kwake wakidai kuwa kuna vurugu zimetokea katika msikiti wa Kitumbini eneo la Majengo, hivyo anahitajika kwenda kutuliza vurugu hizo.
Alisema kwa kuwa alikuwa hawatambui watu hao, isingekuwa vyema kwenda huko kutokana na umbali kwa kuwa kutoka nyumbani kwake hadi kwenye msikiti huo ni zaidi ya kilomita mbili.
Shekhe Chilakwechi alisema baada ya kuwajibu hivyo, watu hao walitoka nje na ghafla kundi jingine la watu lilimvamia kwa kumrushia mchanga usoni na kuanza kumshambulia sehemu kadhaa za mwili.
Alisema wakati watu hao wakiendelea kumshambulia, mke wake alitoka nje na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walitoka na kuanza kuwakimbiza watu hao na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Rajabu Abdallah Likoto (17).
Shekhe huyo alisema mtu huyo alikamatwa baada ya kukwama kwenye matope wakati anavuka mto Mlingoti na alijeruhiwa kwa kukatwakatwa na mapanga. Mtuhumiwa huyo naye amelazwa katika hospitali hiyo
Chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment