Tuesday, 9 October 2012

Uchaguzi UVCCM wajumbe wachapana makonde, mawe

Uchaguzi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Mara, jana uliingia dosari baada ya kuzuka vurugu kubwa na wajumbe kurushiana ngumi, viti, mawe na silaha mbalimbali ndani ya ukumbi.

Mapigano hayo makali yaliyochukua takribani dakika 10, yalisababishwa na kilichodaiwa na wafuasi wa mmoja wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa umoja huo kumvamia Katibu Msaidizi wa CCM wilayani Tarime, Denis Zakaria, na kuanza kumshushia kichapo kwa madai kuwa alikuwa akiwahonga fedha wajumbe wa mkutano huo.

Kufuatia madai hayo, wafuasi hao waliendelea kumzonga Katibu huyo huku wakimueleza kuwa kama amekwenda kwenye uchaguzi huo kwa lengo la kugawa fedha nao walikuwa wakizihitaji.

Baada ya hali hiyo, wajumbe wa mkutano huo kutoka wilayani Tarime walilazimika kutoka nje ya ukumbi, kisha kuanza kupambana na wafuasi hao kwa kurushiana ngumi, mawe na viti huku katibu msaidizi huyo wa CCM wilayani Tarime akitimua mbio na kuingia kwenye ofisi ya Katibu wa CCM wa mkoa ili kunusuru maisha yake.

Kutokana na vurugu hizo, wajumbe hao walionekana kujawa na hasira huku wakimkimbiza kwa mbio katibu huyo msaidizi, ambaye baadaye alifanikiwa kuingia na kujifungia ndani ya ofisi ya CCM mkoa huo.

Baada ya Katibu huyo kujificha ndani ya ofisi akikwepa kipigo, wajumbe hao waliokuwa na hasira walimgeukia na kutaka kumnyang’anya kamera mwandishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Mara, Mabere Makubi, kwa madai kwamba amepiga picha za vurugu hizo.

Baadhi ya wajumbe hao walioonekana kumzonga kwa kutaka kumpokonya kamera mwanahabari huyo, lakini walishindwa kutimiza lengo lao hilo baada ya Makubi kuwakabidhi kamera yake ili watoe mkanda wa picha ya video waliokuwa wakiuhitaji, jambo ambalo walishindwa kisha kuondoka na hasira zao.

Mmoja wa watu walionusurika na kipigo cha vijana hao, Arafat Idd kutoka Wilaya ya Musoma Mjini, alimlalamikia mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa UVCCM Mkoa wa Mara aliyemaliza muda wake, kwa kutaka kuhodhi nafasi zote zichukuliwe na wajumbe wa wilaya ya Tarime.

“Huyu (anamtaja jina) anataka nafasi zote zichukuliwe na watu wa wilaya anayotoka... Makao makuu tunaomba hili suala walione na kulishughulikia, sisi ni vijana wa mjini na tuna uwezo wa kufanya chochote,” alisema kwa jaziba mmoja wa vijana hao.

Baada ya utulivu kurejea, Dito Manko kutoka Tarime alitangazwa  kuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mara kwa kupata kura 274, akifuatiwa na Machumu Manasa kura 245 huku wagombea wengine wakipata kura mbili na mwingine saba.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment