Monday, 8 October 2012

WALIO MCHAFUA MAFURU (NBC)WAMREJESHA KAZINI!!


Takribani miezi mitatu baada ya kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu zilizokuwa zinamkabili, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Lawrence Mafuru (pichani), amerejeshwa kazini.

Julai 19, mwaka huu, Bodi ya Wakurugenzi wa NBC ilimsimamisha kazi Mafuru, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kiutawala, rushwa na ufisadi zilizokuwa zinamkabili.

Taarifa ya NBC kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam ilimkariri Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Dk. Mussa Assad, akieleza kwamba uchunguzi wa tuhuma hizo umekamilika na hivyo Mafuru amerejeshwa kazini mara moja.

Dk. Assad alisema “ilikuwa mchakato muhimu kwa wadau wote katika biashara yetu, wateja, wafanyakazi, wanahisa, wasimamizi na umma kwa ujumla, kwamba uchunguzi wa kina utafanyika kuhakikisha kuwa utendaji wetu makini unaiendesha benki kwa kuzingatia utawala bora.”

Kwa upande wake, Mafuru ambaye amerejeshwa kazini mara moja alieleza kufurahishwa na kitendo hicho na kwamba uchunguzi huo umeiimarisha benki hiyo na kuiaminisha kwa umma.

“Japokuwa kilikuwa kipindiki kigumu kwa taaluma yangu bado ninaamini kwamba uchunguzi ulikuwa muhimu kwa faida ya taasisi inayosisitiza uongozi bora…haya tunayaweka pembeni na tunatazama mbele kufanya vizuri zaidi kuhudumia wateja wetu,” alisema.

NBC imefanya kazi hapa nchini kwa miaka 45 huku ikiwa na matawi 53; mashine za fedha 287; vituo 233 vya mauzo; na wafanyakazi 1,400 nchini kote.
Chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment