Pages

Monday, 26 November 2012

JOKATE ATUMIKA KUTAPELI LAPTOP


SASA imeshakuwa ni kawaida kwa watu mbalimbali kutapeliwa kupitia mtandao wa Kijamii wa Facebook na watu wanaotumia majina ya mastaa.
Safari hii limetumika jina la  Miss Temeke 2006, aliyejikita kwenye tasnia ya filamu na kutamba kwenye mitindo kwa kutumia lebo ya kidoti, Jokate Mwegelo kumtapeli mwanafunzi wa kike wa chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo nje kidogo ya mji wa  Morogoro, Ijumaa Wikienda  linakujuza.
Tukio hilo lililotokea hivi karibuni baada ya mwanafunzi  huyo, (jina tunaliminya) kutapeliwa na Jokate ‘fake’ Kompyuta mpakato ‘laptop’ kupitia mtandao huo.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, awali alimuomba urafiki Jokate akiamini ni Jokate halisi, kumbe alikuwa akiwasiliana na Jokate feki.
“Siku moja Jokate aliniambia kuwa anatafuta ma-modo, kuna patna wake aitwaye Mario alikuwa akitokea Kenya na kuniuliza kama ningeiweza kazi hiyo, sikujivunga kwa kuwa hiyo ilikuwa ni mojawapo kati ya ndoto zangu,” alisema.
Baada ya kumkubalia, mwanafunzi huyo alitakiwa kutuma picha ili zionwe na Mario ambaye angefika Dar na baadaye kuelekea Arusha.
Mwanafunzi huyo akafanya kama alivyoagizwa kwa kuziingiza picha hizo kwenye mtandao wa Jokate, baada ya muda akaambiwa kuwa Mario ameziona na amezipenda. 
“Baada ya siku chache Jokate akaniambia kuwa Mario ametokea  kunipenda, hivyo anataka niwe mpenzi wake, nilikataa pamoja na vishawishi vingi hatimaye tukakubaliana kuendelea kufanya kazi tu.”
Mwanafunzi huyo anazidi kusema kuwa, siku nyingine Jokate alimpigia simu na kumwambia kuwa laptop yake imeharibika na Mario hana kompyuta ya kutumia.
“Akaniomba nimuazime laptop yangu ili Mario aitumie mpaka pale yake itakapopona, nilijua Jokate hawezi kuniibia nikamkubalia,” alisema Mwanafunzi huyo.
Siku ya tukio, Jokate alimpigia tena simu mwanafunzi huyo na kumwambia kuwa yeye atachelewa kufika Morogoro na anamtuma Mario chuoni kwao ili ampe laptop kisha watakutana kikaoni.
“Sijui ni kitu gani, baada ya kuitoa laptop yangu, nikahisi kuwa nimetapeliwa, akili zikanijia, nikampigia simu Mario lakini hakupokea, ukweli nilichanganyikiwa hata nyumbani sijawaambia wazazi wangu kilichonipata,” alisema kwa masikitiko.
Mwanafunzi huyo alisema kuwa, Mario akawa hapokei tena simu yake na alipopokea alisema neno moja tu, ‘Usinisumbue’ kisha kuikata.
Alizitaja  namba za Mario kuwa ni 0659 227 229 na mpaka gazeti hili lilipokuwa likienda mitamboni bado simu hiyo ilikuwa ikiita.
Jitihada za mwanafunzi huyo kwenda kwenye kampuni inayohusika na mtandao wa simu hiyo zilidhihirisha kuwa ametapeliwa baada ya  kuambiwa kuwa  mtu anayetumia simu hiyo haitwi Mario bali ana jina lingine.
“Nilijaribu kwenda polisi lakini nao walitaka niwape pesa ili waweze kumsaka mhalifu, kwa kweli sikuwa na pesa nikaona niachane nao,” alisema mwanafunzi huyo.
Hatimaye mwanafunzi huyo  aliamua kutafuta namba ya kweli ya Jokate, alipoipata ndipo alipogundua kuwa mlimbwende huyo hakuhusika  katika kutapeliwa kwake.
Jokate alipoongea na mwandishi wetu alisikitishwa na tukio hilo na kuwataka watu kuwa makini maana wizi huo umeota mizizi.
“Nimeumia sana kwa jina langu kutumika katika utapeli, ninaomba watu wawe makini na wengine waache tabia hiyo ya kutumia majina ya watu maarufu katika michongo yao,” alisema Jokate.
Hivi Karibuni, baadhi ya mastaa wa kike wakiwemo Wema Sepetu, Jacqueline Wolper na Agness Gerald ‘Masogange’ wamekumbwa na matukio ya kuhusishwa na matukio mbalimbali kutokana na majina yao kutumiwa na watu wengine katika mtandao huo.
chanzo:globalpublishers

No comments:

Post a Comment