Monday, 26 November 2012

Wanaomaliza vifungo hawataki kuishi uraiani


Idadi kubwa ya wafungwa wanaomaliza muda wa kutumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali nchini wanashindwa kukaa uraiani badala yake wanafanya mbinu za kurejea kwenye magereza.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Dk. Immanuel Nchimbi wakati akizindua karakara ya kutengezea magari pamoja na namba mpya za magari katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam jana.
Alisema katika utafiti imebainika kati wa wafungwa 100 wanaomaliza muda wao wa kifungo, 35 wanarudi tena gerezani baada ya kufanya vitendo vya kihalifu kwa makusudi .
Dk. Nchimbi alisema sababu kubwa inayosababisha kukithiri kwa hali hiyo ni tatizo la Jeshi la Magereza kutoweka kipaumbele kuwarekebisha kwa kuwapa mafunzo mbalimbali ya ufundi ili wanaporejea uraiani wawe kazi ya kufanya.
"Wimbi la watu wanaomaliza kifungo chao na kurejea tena gerezani linazidi kukua, kibaya zaidi watu hawa wanafanya makosa kwa makusudi wakijua watafungwa gerezani baada ya kushindwa kuishi kutokana na kutokuwa na kitu cha kufanya," alisema Dk. Nchimbi.
Hata hivyo, alisema uanzishwaji wa karakara ya magari ndani ya Gereza hilo utatoa nafasi kwa wafungwa kujifunza ufundi na watakapomaliza kifungo wataendeleza kazi hiyo.
Hata hivyo, Dk. Nchimbi alisema mradi huo wa utengenezaji wa magari uonyeshe mwanga wa utumishi bora wa Jeshi kwa magari yanayopelekwa hapo na taasisi mbalimbali za Serikali yatengenezwe kwa muda unaokubalika na gharama nafuu.
Alisema imekuwa kawaida kwa miradi mingi ya Serikali kuwa na nguvu ya soda kwa kufunguliwa kwa mbwembwe kubwa, lakini inapoanza kazi haidumu kwa siku nyingi na kuzusha malalamiko kwa wateja.
"Nimeona hapa mradi huu tunauzindua kwa mbwembwe lakini sitegemei ndani ya mezi sita mambo yanakuwa mabaya, imani yangu mtazidi kutuonyesha kuwa miradi yote inayoanziushwa na Jeshi inakuwa bora," aliongeza kusema.
Waziri Dkt. Nchimbi alisema kuna haja kwa sheria ya manunuzi ya Serikali kuangalia upya kwani nyingi haziendi na wakati na kusababisha ukwamaji wa vitu mbalimbali.
Akizungumzia namba mpya za magari za Magereza zinazoanzia na maneno ya MT, Waziri huyo alisema uamuzi huo unalenga kulitambulisha rasmi na kuweka uwazi kwa wananchi wote.
Awali kamishna Mkuu wa Magereza, John Minja alisema kuanzishwa kwa karakana hiyo kutaongeza kasi ya utendaji kazi kwa askari kurekebisha wafungwa kwa vitendo pamoja na kurahisisha jeshi hilo pamoja na Taasisi za Serikali kutumia pesa nyingi kutengeneza magari kwa taasisi zingine.
Aidha alisema namba za magari zimeanza kutumika baada ya waziri husika kuridhia kifungu namba 114 sura 168 ya usalama barabarani kama alivyopewa jukumu hilo kisheria.
Chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment