Saturday, 4 May 2013

M’BILIA BELL: Wivu wa mapenzi ulimkimbiza kwa Tabu Ley



M’BILIA Bell ni mwanamuziki aliyeonesha ujasiri kwa kukataa kuolewa na waziri katika serikali ya nchi ya Gabon, Afrika Magharibi, aliyempa sharti la kuacha muziki ili amuoe.
Bell ni mama aliyejaliwa kuwa sura, umbo lililojengeka lenye mvuto, sauti nzuri ya uimbaji na hata uchezaji wake jukwaani.
Ni mwanamuziki mwenye sifa adimu, ambazo pengine yawezekana zisifikiwe na mwanamke mwingine.
Sifa nyingine kubwa aliyonayo mwana mama huyo ni kuwa, aliolewa na mwanamuziki nguli, Tabu Ley na ndoa yao ya kifahari ilifungwa ndani ya ndege wakiwa hewani.
Jina lake halisi ni Marikirala Mboyo, ambaye kama walivyo watoto wengine wa Kiafrika, wafikiapo miaka minane, hukaa na wazazi, babu au nyanya zao na kulazimishwa kusikiliza hadithi, pia kuimba nyimbo za asili inayowazunguka.
M’bilia alikuwa mmoja wa hao, baada ya kuvutiwa na sauti ya babu yake, ambaye alikuwa bingwa wa kuimba, wakati bibi yake alikuwa mchezaji wa ngoma asiyeshindwa kijijini humo.

Marikirala M’bilia alizaliwa mwaka 1959 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na alianza kuimba akiwa na miaka 17 akiwa na mkongwe Abeti Massekini mwaka 1976.
Akiielezea historia yake, Bell anasema, alianza kupenda muziki baada ya kuangalia katika televisheni na kumuona mwanamuziki nyota kutoka nchi ya Togo, Bela Bello, aliyekuwa akifanya onesho katika mji wa Kinshasa DRC.
Anasema alivutiwa na kipaji cha mwanamuziki huyo na kutamani siku moja aje kuwa kama Bello. Anasema siku aliyosikia kwamba amefariki dunia, alilia kwa siku kadhaa.
Baada ya siku saba kupita, akiangalia televisheni, alimuona mwanamuziki mwingine Abeti Massekini. Baadaye akaamua kumwandikia barua Abeti ya kuomba kujiunga na bendi yake. Alishangazwa kuona Abeti alipomualika kujiunga naye. Hapo ndipo historia katika muziki wake ilipoanzia. Alijifunza kuimba akiwa karibu na Abeti kwa miaka minne.
M’bilia baada ya kujiamini amefuzu, aliondoka kwa Abeti na kwenda kuungana na Sam Mangwana, ambaye aliwasiliana naye baada ya kumuona katika televisheni akifanya vitu vyake. Lakini huko nako hakukaa sana kwani baada ya miaka miwili aliondoka na kujiunga na gwiji la muziki Afrika, Tabu Ley Rochereau mwaka 1981.
Bell alipatwa na mshituko siku aliyokutana na kiongozi wa bendi ya Afrisa International Tabu Ley, akiwa na uso wa furaha katika mahojiano kwa njia ya televisheni.
Ley alimwambia kwamba, hana mabilioni ya kumpatia lakini kama wakifanya kazi pamoja hatajuta kamwe.
M’bilia alitumia mwanya huo akajiunga na bendi ya Afrisa Internationale na ukizingatia sauti yake nyororo, uchezaji wake kupitia maungo yake yaliyojengeka kipekee, kwa kipindi kifupi M’bilia akawa gumzo katika Jiji la Kinshasa. Juhudi zake hizo zilifanya bendi hiyo kuongeza mapato kwa mauzo ya rekodi zao.
Yaelezwa kwamba, M’bilia Bell na Tabu Ley Rochereau walifunga ndoa kabambe ya kifahari wakiwa ndani ya ndege hewani. Katika maisha yao ya ndoa walifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Melodie Tabu, anayesoma jijini Paris na kufanya muziki na baba yake.
M’bilia Bell anamuelezea binti yake huyo kwamba anaongea kwa ufasaha lugha ya Kiingereza na kwamba ni mwimbaji mzuri aliyefuata nyayo za wazazi wake na tayari amemshirikisha katika kuimba kwenye albamu yake mpya ya Belissimo.
Mwaka 1982, Bell alitoka na kibao chake kiitwacho ‘Mpeve ya Longo’, kikisimulia kisa cha mwanamke aliyetelekezwa na mumewe na kuachiwa watoto awalee peke yake. Kibao ambacho kiligusa hisia na kuwa simulizi kila kona za miji ya DRC (zamani Zaire).
M’bilia, aliipenda nchi ya Kenya, alipokuwa katika Jiji la Nairobi, alilazimika kujifunza Kiswahili na kuimba nyimbo kadhaa kwa lugha hiyo.
Nyimbo zilizompatia chati M’bilia zilikuwa za ‘Nakei Nairobi’, ‘Boya ye’, ‘Yamba ngay’, ‘Amour sans frantiere’ na ‘Biu Mondo’.
Mbilia aliimba nyimbo nyingine zaidi za ‘Beyanga’, ‘Befosami’, ‘Faux Pas’, ‘Cadence Mudanda’, ‘Motema’ na ‘Napika’.
Nyimbo za ‘Kuteleza si kuanguka’, ‘Faux Pas’, ‘Iyolela’, ‘Bafosami’, ‘Frontiere’, ‘Phenomene’, ‘Manzil manzil’, ‘Mbanda’ na Nga’, ‘Nadina’, ‘Mayaval’, ‘Eswii yo Wapi’, ‘Biu Mondo’, ‘Nelson Mandela’, ‘Wende na Wende’ na nyingine nyingi zilimjengea heshima Mbilia Bell.
Karibu nyimbo zote alizoimba mwana mama huyo akishirikiana na Rochereau, hazichuji wala kukinai kuziangalia runingani au kuzisikiliza redioni hadi leo.
Mbilia Bell aliwahi kuja Tanzania, akifuatana na mumewe Tabu Ley Rochereau na kundi zima la Afrisa Internationale na alifanya kufuru katika maonesho yao waliyoandaliwa hapa nchini.
Akiwa jijini Dar es Salaam, Bell aliweza kulitawala jukwaa mwanzo mwisho, akitumia kuyachezesha maungo yake sanjari na uzuri wake, akawa kivutio kikubwa.
Tabu Ley, baadaye alimuongeza mwimbaji wa kike, ‘Faya Tess’ ambaye jina lake halisi ni Kishila Ngoyi, akiwa na nia ya kuijenga vema bendi yake.
Lakini ujio wa Faya Tess, ulimfanya M’bilia kuamua kuiacha Afrisa Internationale na kwenda Paris, Ufaransa, ambako alikutana na mwanamuziki wa sokous, mpiga gitaa, Ringo ‘Star’ Bamundele mwaka 1983.
Sababu kubwa za kuondoka kwake ni kile kilichoelezwa kuwa, wivu wa kimapenzi baina ya wana ndoa hao ulioingiliwa na Faya Tess.
Mbilia, aliwahi kuishi nchini Gabon, ambayo inapakana na DRC, ambako alikataa kuolewa na waziri mmoja katika serikali ya nchi hiyo, aliyempa sharti la kuacha muziki ili amuoe.
Anafurahia mafanikio yake na kujivunia kuwa yeye ni mmoja kati ya wanafunzi wa Rochereau Tabu Ley, ambaye alikuwa akimpa kipaumbele na kuwa mwanafunzi bora katika shule yake.
Marikirala Mboyo M’bilia anasema, haikuwa kazi rahisi kukubalika kuwa mwanamuziki mwanamke wa kimataifa katika maisha yake yote ya kazi za muziki. Watu wengi hawakuwa wakimuamini na kuichukulia kazi yake kwamba haitakuwa endelevu.
Bell alikaririwa akisema, kama wao wanawake wanawaamini waume zao na wala hawawalazimishi kuacha kazi zao, iweje wanaume wamfikirie yeye kila anapotikisa maungo yake kwamba huwa anawavutia?
Alitoa wito kwa wanawake wenzake kuungana na kufanya wanaume wawaone kwamba wao hawajirahisishi kama wanavyofikiria.
Marikirala Mboyo ‘M’bilia’, akiwa na muda wa ziada huutumia kufanya shughuli za kijamii, kama vile kuwatembelea watoto wa mitaani, kurekebisha vituo vya watoto hao na kugawa msaada wa vyakula na nguo.
Mwana mama huyo, kwa kawaida huamka kila siku majira ya saa 12:00 asuhuhi na kufanya maombi, baadaye huenda kwenye mazoezi ya viungo. Anatoa siri ya kutochakaa mapema ni kuishi ukiwa na afya njema, wala si kwa kula nyama na kunywa pombe.
Ratiba yake ya asubuhi ni glasi moja ya maziwa isiyokuwa na mafuta, na glasi nyingine maji huwa ndiyo kifungua kinywa chake. Baada ya hapo hutumia muda mwingi katika kuandika nyimbo zake na kuangalia sinema katika televisheni.
Mbilia anasisitiza kwamba, kazi ya muziki ni ya siku nzima na ni ngumu sana, hawezi kupata muda wa kutafuta kazi nyingine kwa kuwa hafikirii kuwa tajiri, ila ameridhika na hali aliyonayo.
Bell ana mpango wa kuwahamsisha wanamuziki wa kike wa Afrika kuungana na wanamuziki wengine kulilia amani.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment