Friday, 3 May 2013

Mjane wa Mwangosi: Namwachia Mungu


IKIWA imetimia miezi tisa tangu kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, mkewe Itika Mwangosi amesema anamwachia Mwenyezi Mungu.
Mwangosi aliuawa kwa kulipuliwa bomu na askari polisi Septemba 2 mwaka jana, wakati akitekeleza majukumu yake kijijini Nyololo, Iringa vijijini katika mkutano wa ufunguzi wa tawi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Hadi sasa ni askari mmoja aliyeshtakiwa kuhusika na mauaji hayo na kesi yake inaendelea katika Mahakama Kuu mkoani Iringa.
Itika ambaye ni mama wa watoto wanne, alisema kuwa Mungu ndiye Jaji Mkuu, na kwamba watuhumiwa wa kifo cha mumewe wanaweza kushinda hapa duniani mbele ya macho ya binadamu wenzao, lakini hawataweza kushinda mbele ya Muumba.
Mjane huyo alitoa kauli hiyo hivi karibuni nyumbani kwake mjini Iringa, alipotembelewa na viongozi na wabunge wa CHADEMA, wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa ili kumjulia hali na kujua maendeleo ya familia yake.
Dk. Slaa anamsomesha mtoto mmoja wa marehemu Mwangosi aitwaye Herzegovina, jukumu alilolichukua baada ya mazishi ya Mwangosi mwaka jana.
Mtoto huyo kwa sasa yuko kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Elbeneza iliyoko Nduli mjini Iringa.
Mbali na Dk. Slaa, viongozi wengine ni wabunge wane; Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini),Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Hyness Kiwia (Ilemela).
Akitoa maelezo juu ya maendeleo ya familia yake, hususan mtoto anayesomeshwa na Dk. Slaa, mjane huyo alisema anaendelea vyema.
“Herzegovina anaendelea na masomo yake shuleni, wenzake; Nehemia aliyemaliza kidato cha nne, Bathsheba aliye darasa la tano na Moria mwenye miaka mitatu nao wanaendelea vyema.
“Kwa ujumla familia yote ipo, tunaendelea kuzoea maisha haya mapya... kwa kweli tunashukuru sana kwa msaada wako wa kumsomesha Herzegovina,” alisema mjane huyo.
Akijibu swali la Mbilinyi ambaye ni Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, aliyetaka kujua anaonaje namna tukio la kifo cha mumewe linavyoshughulikiwa, Itika alisisitiza kuwa; “kwa kweli nimemwachia Mungu.”

Mmoja wa ndugu zake, aliyetajwa kwa jina moja la Suzy, alisema kuwa tangu kuuawa kwa Mwangosi na namna tukio hilo linavyochukuliwa na mamlaka husika, vikiwemo vyombo vya dola, imekuwa ikiwasikitisha sana na kuwafanya wajenge chuki na watawala.
chanzo:daima


No comments:

Post a Comment