Saturday, 4 May 2013

Mwandishi wa habari avamiwa, avunjwa mguu

Mwandishi wa habari wa magezeti ya NIPASHE na The Guardian mkoani Shinyanga na Simiyu, Aniceth Nyahore amevamiwa na kushambuliwa kwa nondo na kuvunjwa mguu wake wa kulia.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya serikali ya mkoa wa Shinyanga alikolazwa kwa ajili ya matibabu, Nyahore alisema alikumbwa na mkasa huo juzi majira ya saa 4.30 usiku kwenye barabara ya Uhuru maeneo ya karibu na nyumba ya kulala wageni ya Urambo na baa maarufu ya Papilon mjini Shinyanga.

Alisema pamoja na watu hao wanaosakiwa kuwa sita kumvamia na kumvunja mguu, pia walimpora fedha zote alizokuwa nazo kiasi cha Sh. 120,000, simu yake ya mkononi aina ya Nokia na Modemu ya mawasiliano kwa njia ya mitandao aina ya Zantel.

“Nilikuwa natoka kuchukuwa fedha hizo kwa wakala wa M-Pesa maeneo ya Ryamisaga karibu na ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga mjini nikirejea nyumbani nilipofika maeneo hayo ghafla nikazungukwa na watu kama sita hivi na kuniambia uko chini ya ulinzi," alisema.

“Nikiwa bado nawaangalia mmoja wao akasema kaa chini nikakaidi amri hiyo ndipo wakanishambulia kwa nondo mguuni na kunivunja hatimaye wakanipora vitu vyote nilivyokuwa navyo mifukoni mwangu na kuniacha nikigalagala chini nikitafuta msaada kwa wapita njia” alisema.

Nyahore alisema alifanikiwa kuokotwa na wasamaria baada ya kupiga kelele akiomba msaada ambao walimchukua na kupelekwa hospitalini hapo.

Mmoja wa madaktari wa mifupa hospitalini hapo ambaye hakutaka jina lake litajwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa Nyahore amevunjika vibaya mguu huo chini karibu na jicho la mguu (kwenye ugoko) hali aliyosema inatia shaka kuungwa kwake na anastahili kutibiwa kwenye hospitali yenye vifaa vya kisasa.


Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarst Mangalla, alikiri kupokea taarifa za awali kuhusiana na tukio hilo na kwamba polisi inalifanyia kazi tukio hilo
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment