Friday 16 December 2011

PENGO AZUNGUMZIA USHOGA


Afadhali tunyimwe hiyo misaada kuliko uendawazimu

 ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, jana aliweka tena msisitizo wa kukataa misaada kwa masharti ya kuruhusu ndoa za mashoga nchini.
"Mungu aliwaumba mke na mume kwa hisia ili washiriki tendo la ndoa na kuongeza familia, kama hivyo ndivyo, iweje wanaume kwa wanaume au wanawake kwa wanawake waoane wakati wakijua kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Mwenyezi Mungu? 
Suala la ushoga, kwangu nalitazama jambo hilo kama uendawazimu," 

“Nasifu msimamo uliooneshwa na viongozi wetu wa kukataa mawazo ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kuzilazimisha nchi zikubali ndoa za mashoga kwa sharti la kupewa misaada. Afadhali tunyimwe hiyo misaada kuliko uendawazimu,” alisema Pengo.

Pia alifichua kile serikali ilichokifanya wakati wa kukusanya maoni ya wadau mbalimbali kuhusu  muswada wa uundwaji wa Katiba mpya.
Kardinali Pengo alisema serikali haikuwa na lengo la kupata maoni ya wadau muhimu, na ndiyo maana ilitoa muda mfupi kuliko ilivyotarajiwa.
Pengo, aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Kanisa Katoliki la Mt. Joseph, alisema alishangazwa na hatua ya serikali ya kumpa muda wa siku nne kutoa maoni yake, huku ikijua kuwa alikuwa nje ya nchi kikazi.
Alisema yeye kama kiongozi wa taifa, haikuwa busara kwake kupewa muda wa siku nne kujaza fomu ya maoni. Akauliza iwapo yeye alifanyiwa hivyo, ilikuwaje kwa watu wengine wa kawaida.
Kardinali Pengo alisema aliletewa barua Novemba 30 mwaka huu akiombwa kutoa maoni yake kwa maandishi na kutakiwa kuyawasilisha kabla ya Desemba 4.
Alisema kutokana na majukumu mengi aliyonayo alishindwa kutimiza sharti hilo kwa vile alikuwa safarini nje ya Dar es Salaam.
“Lakini hata ningekuwepo bado nisingeweza kufanya hivyo ndani ya muda huo wa siku nne kulingana na majukumu mengi niliyonayo,” alisema Pengo.
Aliongeza kuwa uzembe huo uliofanywa na serikali, ndio uliosababisha machafuko katika mataifa mengi kutokana na watawala kufanya jambo hilo muhimu kwa uzembe.
“Lazima tutambue kuwa katiba ni chombo muhimu ambacho kinatuongoza, Rais akichaguliwa lazima aapishwe kwa katiba ili aweze kuilinda. Sasa tumebakiza miaka minne kufika uchaguzi mwingine, kwa kuzembea huku tutajikuta njia panda.
…najua huko mbele tukikwama wanaweza kusema rais aendelee hadi katiba mpya ikamilike, lakini itabidi aapishwe, sasa ataapa kwa katiba ipi…hii ambayo tunaikataa kuwa haifai ama mpya ambayo itakuwa haijakamilika?” alihoji Kardinali Pengo.
Alionya na kuitaka serikali kusimamia kikamilifu bila hila wala uzembe upatikanaji wa Katiba itakayokubaliwa na wengi, vinginevyo kuchelewa kwao kutaliweka taifa katika wakati mgumu.

Mbali na kufichua siri hiyo, Kardinali Pengo amewashukia Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa hatua yake ya kujiongezea posho, akisema hiyo ni dalili ya kushindwa kuwatumikia wananchi wanyonge.
Mwadhama Pengo alisema kiongozi anayejali maisha ya watu kamwe hawezi kujifirikia mwenyewe, lakini katika tukio la posho za wabunge, ameshangazwa na uamuzi wa Spika wa kuongeza posho za wabunge.
“Hivi karibuni tumesikia wabunge wetu wameongezewa marupurupu ya posho wakidai hali ya maisha imekuwa ngumu wala hawakujali ugumu wa maisha waliyonayo wananchi wanaowaongoza. Najiuliza huyu kiongozi ni wa namna gani anayejifikiria yeye kwanza kabla ya wengine?” alihoji Kardinali Pengo.

Alisema wabunge ni wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kushughulikia matatizo yao, hivyo hawapaswi kutumia mamlaka yao kujipangia marupurupu manono wakati wakijua wale wanaowaongoza wana maisha magumu.
Alisema kuwa Wakristo wanaamini kuwa Yesu Kristo alizaliwa kama maskini kwenye familia duni licha ya kwamba ni mwana wa Mungu, ikiwa ni ishara ya kupeleka ujumbe kuwa alikuja kwa ajili ya wanyonge, jambo alilosema linapaswa kuigwa na viongozi.
Alisema ujumbe wake kwa viongozi wote katika sikukuu hizi ni kuwataka wajenge moyo wa kuwafikiria kwanza wale wanaowaongoza kabla ya kujinufaisha wao kama alivyofanya Yesu Kristo.
Kauli ya Kardinali Pengo kuhusiana na suala la Katiba na Posho ni msumari mwingine wa moto kwa serikali, baada ya kelele na upinzani mkubwa kutoka kwa Watanzania wa kada mbalimbali waliopinga vikali mchakato mzima wa kukusanya maoni ya kuundwa kwa muswada wa Katiba mpya.
Aidha, kauli ya Pengo juu ya posho za wabunge imeshindilia zaidi upinzani mkubwa ulioibuliwa na wabunge wa Chadema na wa wananchi waliopinga hatua ya Spika wa Bunge kuongeza posho ya vikao kwa wabunge.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitangaza ongezeko la posho ya vikao vya wabunge kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 ambayo alisema imeanza kulipwa tayari.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alikataa kupandishwa kwa posho hizo kwa kuwa rais hajaidhinisha.

No comments:

Post a Comment