Thursday, 10 May 2012

MBARONI AKITUHUMIWA KUMUUA SHEMEJI YAKE!!

POLISI mkoani Arusha wamemkamata mkazi wa Pinyinyi wilayani Ngorongoro, Kumari Nangau (45) kwa tuhuma za kumuua shemeji yake Namoronjo Mollel (45) kwa kumpa pombe inayodhaniwa kuwa ya sumu. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alisema Mollel alifariki saa 7:30 mchana juzi katika kijiji cha Pinyinyi wilayani Ngorongoro. 

Uchunguzi wa awali wa Polisi ulibaini kuwa kifo hicho kilitokana na ugomvi wa siku nyingi kutokana na Nangau kumdai Mollel Sh 230,000 kwa siku nyingi. 

Alidai kutokana na deni hilo kukaa kwa muda mrefu bila kulipwa ndipo, Mollel alipoamua kumchukua mke wake ambaye alikuwa ndugu yake Nangau na kumrudisha kwao mpaka atakapofanikiwa kulipa deni hilo kwa kuwa lilisababisha ugomvi ndani ya nyumba. 

Hata hivyo Mollel alijitahidi kulipa deni hilo ili arudishiwe mke wake lakini wazazi wa mwanamke hawakukubali mtoto wao arudi kwa mume wake kwa wakati huo baada ya kuwa na wasiwasi wa tabia ya mwanamume huyo. 

Alisema siku ya tukio, Mollel akiwa na mwenzake walikwenda kwenye klabu ya pombe za kienyeji wakaagiza pombe ambayo ililetwa na Nangau ikiwa katika vikombe tofauti. 

Alisema baada ya Mollel kunywa pombe hiyo, hali yake ilibadilika na akaomba maji ya kunywa watu wakamshauri apewe maziwa lakini kwa bahati mbaya alifarikiKamanda Andengenye alisema baada ya kutokea kwa kifo hicho Nangau alitaka kukimbia lakini watu waliokuwa katika eneo hilo walifanikiwa kumkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi wilayani Ngorongoro. 

Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi Hospitali Teule ya Waso na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi. Polisi wanaendelea kumhoji mtuhumiwa na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
                                        NA HABARI LEO

No comments:

Post a Comment