Thursday, 20 September 2012

CHADEMA YAWAKILISHA BARUA KWA KIKWETE.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimwandikia barua  Rais Jakaya Kikwete, kikimuomba kuunda tume huru ya kimahakama kwa lengo la kuchunguza vifo vyenye utata vinavyotokea kwenye mikutano ya kisiasa na maandamano nchini.

Aidha Chadema, kimemuomba Rais achukue hatua ya kuwafukuza kazi viongozi waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na ongezeko la mauaji hayo ambayo baadhi ya  watuhumiwa ni Jeshi la Polisi.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi  Chadema, John Mnyika, alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa, kuna haja ya kufanyika uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano na mazingira ya kisiasa.

Katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu watu kadhaa walifariki kwenye matukio ya kisiasa. Waliouawa na idadi kwenye mabano ni Arusha Mjini (watatu), Igunga (mmoja), Arumeru Mashariki (mmoja), Iramba (mmoja), Morogoro (mmoja) na Iringa (mmoja).

Taarifa ya Chadema ilisema kuwa barua hiyo iliandikwa Septemba 10, mwaka huu na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na kwamba amemuomba Rais Kikwete kuchukua hatua ya kuwafukuza kazi viongozi waandamizi wa serikali na Jeshi la Polisi.

Mnyika alisema kuwa waliopendekezwa kufukuzwa kazi ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema.

Viongozi wengine ambao chama hicho kimependekeza wafukuzwe ni  Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja; Kamanda wa Polisi  wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

Mbowe katika barua yake hiyo amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho wakati Chadema kikisubiria majibu ya barua hiyo kutoka kwa Rais, wasitoe ushirikiano kwa timu iliyoundwa na Dk. Nchimbi kuchunguza mauaji ya kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na nyingine ambazo zimeundwa kuchunguza vifo vyenye utata.

Chama kimeainisha matukio ya mauaji yaliyotokea mwaka jana na mwaka huu katika harakati za kisiasa kuwa ni pamoja na lile la Januari 5, mwaka jana ambalo watu watatu waliuawa na polisi jijini Arusha wakati wa kuvunja maandamano ya wanachama na wapenzi wa Chadema ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa umeya wa Jiji hilo.

Mnyika alisema wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, mwanachama wa Chadema, Mbwana Masoud, aliuawa kwa kunyongwa katika mazingira ya kutatanisha.

Kiongozi wa kata wa Chadema, Msafiri Mbwambo (32), alichinjwa na chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kusababishwa na masuala ya kisiasa baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Julai 15, mwaka huu mkoani Singida Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa Kata ya Ndago, wilayani Iramba, Yohana Mpinga (30) aliuawa katika vurugu baina ya CCM na Chadema baada ya kumalizika kwa mkutano wa Chadema.

Mjini Morogoro, Agosti 27, mwaka huu  polisi walimuua kwa risasi mkazi mmoja wa mjini humo aliyedaiwa kuwa ni muuza magazeti, Ally Nzona, wakati wakivunja maandamano ya Chadema kabla ya kufanyikwa kwa mkutano wa hadhara.

Tukio lililotikisa sana nchi ni la mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliyeuawa na Polisi waliovamia ufunguzi wa tawi la Chadema katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi, mkoa wa Iringa.

Mnyika alisema kuwa licha ya mauaji hayo kulalamikiwa na wananchi, bado hakuna uchunguzi wa kimahakama uliofanyika.

chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment