Wednesday, 19 September 2012
MASTAA WATIBUANA MAKABURINI!!!!!
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mastaa wa filamu Bongo wametibuana wakiwa ndani ya eneo la Makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mastaa hao walifika eneo hilo kuungana na ndugu, jamaa na marafiki wengine kwenye maziko ya mtoto wa msanii mwenzao, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ aliyekuwa akiitwa Wighton Steven.
Mtoto Wighton alifariki ghafla siku nne baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Mwanyamala jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa mara baada ya kuzaliwa.
Baada ya kukamilisha zoezi la kumsitiri mtoto Wighton, baadhi ya mastaa walihamishia msiba katika kaburi la staa wa filamu za Kibongo, Steven Kanumba ambapo vilio vilianza upya.
Wakiendelea kulia juu ya kaburi la Kanumba, kijana mmoja ambaye jina lake halipatikana mara moja anayedaiwa kuanza kufurukuta kwenye filamu, aliwajia juu na kuwaita wanafiki kwa vile hawana upendo wa dhati na marehemu Kanumba.
“Hamna lolote nyinyi (akiwasonza kidole), mnalia unafiki tu...kama siyo huu msiba mngekuja saa ngapi kulia juu ya kaburi lake? Kama kweli mnampenda, kwa nini msichange fedha na kuweka marumaru kwenye kaburi lake badala ya kuja kulialia uongo?
“Tangu amezikwa hapa mmewahi kuja hata mara moja? Hata mlinzi mwenyewe (wa makaburini pale) anaeleza wazi....anayeonekana hapa mara kwa mara ni Steve Nyerere na Wolper (Jacqueline) ambaye alifika mara moja kufagia, haya nyie vipi?” alisema kijana huyo akionekana kuwakamia sana.
SHILOLE AJIBU MASHAMBULIZI
Maneno makali ya kijana huyo yaliwakera mastaa hao na hivyo kuanza kujibizana naye kwa mtindo wa kutupiana maneno huku wakimsihi aondoke bila mafanikio.
Zuwena Mohamed ‘Shilole’, staa wa filamu anayefanya vizuri kwa sasa kwenye Bongo Fleva, aliamua kuchukua mzigo mzima na kumshambulia kijana huyo anayeelezwa kutaka kutafuta jina kwa nguvu.
“Kwanza wewe ni nani? Huna lolote, hujawahi kuonekana kwenye filamu hata kwenye kisehemu cha kupita tu kwenda dukani...kwenda zako, huna jipya.”
JOHARI ATIMUA MBIO
Mkongwe kwenye sinema, Blandina Chagula ‘Johari’ aliyekuwa amepiga magoti pembeni ya kaburi la Kanumba akilia kwa uchungu, alikerwa na maneno ya kijana yule na hivyo kuamua kuinuka na kutimua mbio huku akiendelea kulia.
Hata hivyo baadaye Johari alitulizwa na wenzake huku jamaa aliyewatibua akiendelea na hamsini zake.
chanzo:http://www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment