Vigogo kadhaa wakiwamo wabunge wameenguliwa katika mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Majina ya vigogo hao yaliondolewa na Kamati ya Maadili iliyoketi mjini hapa kwa siku tatu mfululizo chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Rais Kikwete jana asubuhi alisema kazi ya kupitia majina ua wagombea ilikuwa ni ngumu na kwamba Kamati ya maadili ilifanya kazi nzuri na itafanya vikao vinavyofuata kwenda kwa kasi nzuri.
Akifungua kikao cha Kamati Kuu (CC), Rais Kikwete alisema kuwa Kamati ya Maadili imekuja na mapendekezo mengi tofauti na yale yaliyoliyopendekezwa na vikao vya mikoani.
Rais Kikwete alisema Kamati ya Maadili imefanya kazi ya kupitia jina moja hadi jingine ili kufahamu kwa nini waliochwa kupendekezwa wamefanyiwa hivyo.
“Tumefanya kazi ya kupitia jina moja hadi jingine kuona nani amependekezwa na wasiopendekezwa na kwa nini wameachwa na kuna maeneo tumekuja na mapendekezo tofauti na yaliyotolewa mikoani kwa sababu mbalimbali,” alisema.
Alisema wagombea 2,853 waligombea nafasi mbalimbali ndani ya chama na wengine 2,104 waliwania mafasi za uongozi kupitia jumuiya za chama hicho.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho ambazo imelifikia gazeti hili jana, zilisema kuwa waliodaiwa kuenguliwa na kikao hicho ambacho kilimalizika juzi saa 9:30 usiku, ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, anayetetea nafasi yake.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe anayewania nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama hicho (UWT) mkoani Tabora na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Kada mwingine ambaye taarifa za uhakika zinaeleza ameenguliwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani Dodoma, Antony Mavunde, ambaye anagombea Makamu Mwenyekiti Taifa.
Habari zaidi za uhakika zinasema kuwa wengine ambao majina yao yameondolewa katia orodha ya wagombea ni wabunge Victor Mwambalaswa (Lupa) na Godfrey Zambi ( Mbozi Mashariki).
Zambi na Mwambalaswa walikuwa wanagombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.
Hata hivyo, chanzo chetu kimesema kuwa kuna vigogo wengine ambao wamependekezwa waenguliwe na hivi sasa wanasubiri huruma ya vikao vya CC na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi wabunge waliowania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama, majina yao yamepitishwa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CC imekuwa ikitumia busara katika kupitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali kwa maslahi ya chama.
“Hata kanuni inasema kuwa anaweza kugombea kwa kibali maalum cha Kamati Kuu. Majina yanapofika tunasema huyu ni mbunge, tunaangalia je, inafaa tena kugombea nafasi nyingine inaporidhika basi inatoa kibali kwa mtu kuwania nafasi ya uongozi,” alisema.
Alisema CC imewahi kuruhusu na kukataa maombi ya watu mbalimbali kwa hivyo hilo halitakuwa jambo geni kama litatokea katika vikao vinavyoendelea.
Chanzo hicho kilisema kuwa Kamati ya Maadili iliamua kurahisisha kazi ya vikao hivyo kwa kuchambua jina moja baada ya jingine na kutoa mapendekezo yao kulingana na sifa walizonazo wanaomba kugombea nafasi hiyo.
Nape alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusiana na taarifa za vigogo hao kuenguliwa, hakudhibitisha wala kukanusha taarifa hizo zaidi ya kusema kuwa hayo ni maneno ya barabarani.
Pia Nape aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa vikao hivyo siyo vya mwisho kutoa maamuzi na kuwa maamuzi hayo yanaweza kubadilishwa na vikao vingine.
Kikao cha mwisho kutoa maamuzi ni NEC ambacho kinatarajiwa kuanza leo.
CHEGENI, KAMANI WAWAGAWA VIJANA BUSEGA
Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM) Wilaya ya Busega, imeingia katika mvutano baada ya mwenyekiti wake, Samuel Ngofilo, kutoa kauli yenye utata.
Moja ya kauli hizo ni kwamba vijana wamemchukulia fomu ya kugombea ujumbe wa NEC, mbunge wa zamani wa Busega, Dk. Raphael Chegeni.
Viongozi wa umoja huo wameitisha mkutano wa waandishi wa habari na kumkana mwenyekiti wao wakisema huo ni uongo na uzushi na kumtaka awaombe radhi.
Katika mkutano huo kwenye mji mdogo wa Lamadi jana, vijana hao ambao ni wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Wilaya ya Busega, walidai kuwa kitendo cha mwenyekiti wao kuzungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa kuna njama zimesukwa za kutaka jina la Dk. Chegeni likatwe kwenye kugombea nafasi hiyo ya ujumbe wa NEC pia ni uzushi.
Pia walidai kuwa wameshangazwa na Ngofilo kumtuhumu Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani, kwamba aliandika barua kwenda kwa katibu wa CCM mkoa wa Mwanza, akiomba jina la Dk. Chegeni lisipitishwe kwenda ngazi ya Taifa.
Wakiongozwa na Juma Kaduka pamoja na Muddy Gimonge, walisema wakiwa kama wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya vijana wilaya ya Busega, wanashangaa sana kwa kauli tata za mwenyekiti wao na kwamba anataka kuwagawa vijana.
Walisema kuwa kauli ya mwenyekiti wao hazikupitia kwenye vikao halali vya baraza au kamati ya utekelezaji UVCCM ya wilaya.
“Tunakanusha vikali kwamba sisi kama vijana tulimchukulia fomu Dk. Chegeni za kugombea NEC kama mwenyekiti wetu alivyotangaza kwenye vyombo vya habari,” alisema Gimonge.
Aliongeza: “Lakini pia mwenyekiti wetu amedai kuwa Dk. Kamani ameandika barua kwenda kwa katibu wa CCM mkoa eti jina la Dk. Chegeni likatwe kwenye kinyang’anyiro cha NEC, huo pia ni uzushi sisi kama vijana hatulijui jambo hilo.”
Walisema kumuingiza Dk. Kamani katika mambo hayo ni kumuonea kwa sababu yeye siyo mgombea katika kinyang’anyiro cha NEC.
Walisema kuwa katika kikao chao cha juzi kilichoketi katika kijiji cha Nyang’anga Kata ya Nyashimo, Baraza la UVCCM lilikuwa na ajenda moja ya kukamilisha uchaguzi wa Kamati ya Utekelezaji ya Wilaya ya Busega na wala hawakuwa na ajenda tofauti na hiyo.
Juzi Mgofilo alikaririwa na vyombo vya habari akitoa kauli hizo, ikiwemo ya kusema kuwa vijana wa CCM wilayani hapa ndiwo waliomchukulia fomu Dk. Chegeni ya kugombea NEC na pia Dk. Kamani ameandika barua kwenda kwa katibu wa CCM mkoa wa Mwanza ili jina la Dk. Chegeni likatwe.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment