Monday, 17 September 2012

NI MABOMU,RISASI UCHAGUZI BUBUBU!!!!

Risasi za moto, uharibifu wa mali, kupigwa mwandishi wa Channel Ten Zanzibar, ni miongoni mwa mambo yaliyotawala katika zoezi la uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu uliofanyika jana mjini Zanzibar.

Uchaguzi huo mdogo ulifanyika kuziba nafasi iliyokuwa wazi baada ya kufariki dunia kwa Mwakilishi wa zamani wa jimbo hilo, Salum Amour Mtondoo, Februari, mwaka huu.

Vurugu zilianza kutokea mapema baada ya kufunguliwa vituo saa 1:00 asubuhi, ambapo katika kituo cha Beitrasi, risasi za moto zilipigwa na watu waliokuwa wamevaa nguo za kiraia, na kufunika nyuso zao kwa vitambaa vyeusi na vyeupe wakiwa katika gari aina ya Toyota Pick Up.

Watu hao waliteremka kabla ya gari kusimama na kurusha risasi tatu hewani na kusababisha watu kukimbia hovyo.

Askari hao walifika katika eneo hilo saa 7:00 mchana na kutawanya kundi la watu waliokuwa wamekaa upande wa pili wa mlango mkuu wa vituo vya wapiga kura, wakifuatilia watu wanaoingia na kutoka waliopakiwa kwenye magari wakiwa chini ya uangalizi wa askari wa vikosi vya SMZ.


Watu kama hao pia walitawanywa katika kituo cha Bububu baada ya kuibuka watu waliokuwa wakiyapekua magari na kuwahakiki waliokuwemo kabla ya kuelekea katika vituo vya wapiga kura, jambo ambalo lilisababisha watu wengi kushindwa kwenda kupiga kura kwa utaratibu wa kusafirishwa kwenye magari maalum.


Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya watu waliokuwa nje ya vituo wakizuia watu kwa kuwatuhumu kuwa ni mamluki, walisema kwamba haiwezekani mkazi halali wa jimbo apelekwe kwa magari wakati vituo vipo mita chache kutoka maeneo wanayoishi.

“Hawa wanaokuja ndani ya magari hatuamini kama ni wakaazi wa Bububu, ndiyo maana tunazuia magari kuingia katika vituo vya wapiga kura na watu,” alisema Rashid Juma, mkazi wa Beitrasi.

Wakati waandishi wakitoka katika kituo cha Beitrasi kuelekea Bububu, walikuta gari eneo la Kibweni likivunjwa vioo kwa kutumia mawe na magongo kisha kuendeshwa na kuligonga katika vikuta vilivyopo pembezoni mwa barabara kabla ya kurudi nyuma mbio na kuligonga gari la abiria.

Gari hilo aina ya Toyota Vitz lenye namba za usajili Z 979 DR, lilifanyiwa uharibifu mkubwa mkabala na Ikulu ndogo ya Kibweni, ambapo Mwandishi wa Channel Ten Zanzibar, Munir Zacharia, aliegesha gari lake pembeni na kushuka kupiga picha, lakini ghafla alivamiwa na kundi la  vijana waliokuwa wamekusanyika nje ya tawi la CCM na kuanza kumpiga ngumi na kumjeruhi mdomo na sehemu ya bega.

"Mnyang’anyeni kamera, apigwe, hapana mwacheni, toa kaseti hiyo, futa mkanda huo,”  zilisikika sauti za vijana hao kabla ya askari Polisi waliokuwa katika gari  PT 1449, kufika eneo hilo na kumwokoa mwandishi huyo kisha wakampakia katika gari lao na kuondoka naye.

Askari hao baadaye walilichukua gari la mwandishi huyo aina ya Toyota Spacio lenye namba za usajili Z 623 DR na kumuondoa katika eneo la tukio kwa usalama wake.

Juni 2, mwaka huu, mwandishi mwingine wa kituo hicho cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kupigwa bomu akiwa kazini katika kijiji cha Nyololo Wilaya Mufindi mkoani Iringa.

Akizungumza na NIPASHE, Zacharia alisema kamera imeharibiwa, pochi imeibiwa na kupigwa ngumi mdomoni na mabegani. Alisema alikwenda kuripoti kituo cha Polisi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za matibabu.

“Nashindwa kuelewa kwa nini wananipiga wakati natekeleza majukumu yangu, hilo ni tukio baya katika misingi ya demokrasia na utawala bora,” alisema Zacharia.

Msimamizi wa Uchaguzi katika kituo cha Beitrasi, Abdullah Bakari Khamis, alisema zoezi hilo lilianza saa 1:00 asubuhi ambapo makundi ya watu yalijitokeza mapema na kupiga kura, lakini wakati wa mchana vituo vingi vilikuwa vitupu, ama vikiwa na wapiga kura mmoja mmoja.

Alisema kituo hicho kilikuwa na vyumba vya wapiga kura wanane na hakukuwa na matatizo yoyote hadi mchana mbali na matukio yaliyokuwa yakijitokeza katika lango kuu la kuingilia kwa kusheheni askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) wakiwa na silaha za moto kuimarisha ulinzi eneo hilo.

Msimamizi wa kituo cha Bububu, Maalim Mussa, alisema hadi mchana zoezi lilikuwa linaendelea vizuri na watu walianza kujitokeza tangu saa 1:00 asubuhi kituoni hapo.

Hata hivyo, alisema majina ya wapiga kura yalibandikwa vituoni wiki moja kabla ya uchaguzi huo, lakini wananchi wengi hawakujitokeza kuyasoma ili kuhakiki na kujua wamepangiwa chumba namba ngapi.

Kutokana na mparaganyiko huo, maafisa wa uchaguzi waliwasaidia kusoma majina yao na kutambua vyumba walivyopangiwa na kuhakikisha watu wote wanapiga kura kama ilivyopangwa.

Matukio hayo yanatokana na mchuano mkali kati ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Makungu na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Issa Khamis Issa, kila upande ukipigania ushindi ambapo wafuasi wa wagombea hao walikuwa na mivutano mikubwa hasa katika suala la wapiga kura halali na wale wanaopakiwa katika magari maalum na kufikishwa katika vituo vya kupiga kura.

Mwangalizi mmoja wa uchaguzi kutoka CCM, Thuwayba Kisasi, alilaani kitendo cha makundi ya watu kuzuia watu wengine kwenda kupiga kura wakati siyo makarani wa uchaguzi wala mawakala wa vyama na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaweza kuwa chimbuko la vurugu.

Mwangalizi wa uchaguzi kutoka CUF, Habib Mohamed Mnyaa, alisema kuna michezo michafu ambayo imetia doa zoezi la uchaguzi huo ikiwemo mtu halali kuingia katika kituo na kukuta jina lake limeshatumika kupigwa kura na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, Mnyaaa ambaye ni Mbunge wa Mkanyageni, alisema jambo la kujiuliza inakuwaje mtu aingie katika kituo cha wapiga kura akiwa na kitambulisho ambacho hakina picha yake na kufanikiwa kupiga kura.

Mgombea wa ADC, Zuhura Bakari Mohamed, alisema atakuwa mzito kuyatambua matokeo kutokana na mkasa alioshuhudia kuwa unakwenda kinyume na taratibu za uchaguzi.

Alisema saa 6:20 yaliingia magari matatu ya vikosi vya ulinzi na usalama yenye namba za usajili 2609 JW 97, 20606 JW 97 na KVZ 109 ambayo yalikuwa yamepakia watu wasiopungua 30 na kutoweka baada ya kukamilisha kazi ya kupiga kura katika kituo hicho.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohamed, hakuwa tayari kuzungumzia matukio ya vurugu likiwemo la kupigwa kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten.

 “Niache nina kazi mkononi,” alisema Kamanda Mohamed, baada ya kupokea simu yake ya kiganjani kisha kuikata.

Kuhusu kuimarishwa askari wa vikosi wakiwa na silaha za moto katika milango mikuu ya kupitia wapiga kura, katika kituo cha Beitrasi na Bububu, Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari, alikataa kuzungumza chochote kwa maelezo kuwa waandishi ni mashuhuda wa matukio hayo.

Abubakar ambaye alikuwepo katika vituo vya kupigia kura akiwa kama Mwangalizi kutoka CUF, alikataa kujibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya kutakiwa kuelezea misingi ya demokrasia na utawala bora katika uchaguzi.

“Nimekwambia sitaki kuzungumza au hufahamu Kiswahili nikueleze kwa Kiingereza?,” Alihoji waziri huyo aliyekuwa akitoka msikitini uliopo kituo cha kupigia kura cha Beitrasi eneo la Chuo Kikuu cha Ualimu cha Nkrumah.

Wakati zoezi hilo lilipokuwa likielekea ukingoni, vurugu ziliendelea kutawala katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, ambapo matairi ya magari yalichomwa moto barabarani na mawe makubwa kutumika kufunga njia karibu na kituo kikuu cha Polisi cha Bububu.

Aidha, risasi za moto nazo zilirindima katika maeneo mbalimbali, kujaribu kuwatawanya watu waliokuwa karibu na vituo wakifuatilia mwenendo wa uchaguzi huo na kuzuia magari yaliyopakia watu katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Wakati tukienda mitamboni, matokeo katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu yametangazwa ambapo mgombea  Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Ibrahim Makungu, ameibuka kidedea kwa kupata kura 3,371.

Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Sululu Rashid Ali, akitangaza matokeo hayo, alisema mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Issa Khamis Issa, alipata kura 3,204  huku mgombea wa Chama cha ADC, Zuhra Bakari Mohamed, akiambulia kura 45.

Alisema wagombea wa vyama vingine na idadi ya kura zao katika mabano ni Jahazi Asilia (7), AFC (6), Tadea (5), SAU (4), Nccr- Mageuzi (3) na NRA kimepata kura moja.

Hata hivyo, wakati wagombea wa vyma vingine wamekubali matokeo hayo, CUF wameyapinga kwa madai kwamba taratibu kadhaa za uchaguzi zilikiukwa.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment