Thursday, 20 September 2012

UNYAMA WA POLISI: MIAKA MITATU FAMILIA ZAOMBOLEZA!!

                                             Mzazi wa Shedrack Motika(Olais Motika)

Miaka mitatu sasa bado familia za vijana waliouawa kikatili na askari polisi mkoani Arusha zinaomboleza huku zikisubiri haki itendeke kwa waliohusika kukatisha maisha ya watoto wao kuchukuliwa hatua za kisheria.

Majonzi hayo yakiwa yamegubika familia hizo, kesi dhidi ya askari polisi wanaotuhumiwa kuwaua vijana hao haijapelekwa mahakamani miaka mitatu tangu tukio hilo litokee na hakuna dalili yoyote kwamba hatua zitachukuliwa.

Tukio la vifo vya Ewald Mtui na Shedrack Motika wanaodaiwa kukatishwa maisha yao na risasi za polisi katika mazingira ya utatanishi wakidaiwa kuwa ni majambazi waliokuwa wanataka kupora kwenye  kituo cha mafuta eneo la Kijenge, linaendelea kutesa mioyo ya wapenda haki, ndugu na jamaa wa vijana hao.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, wana familia hizo wamedai kuwa serikali imeshindwa hata kuwapeleka mahakamani askari wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo yaliyotikisa Jiji la Arusha na vitongoji vyake.

Mzazi wa marehemu, Motika, Olais Motika alisema kuwa wamelifuatilia suala hilo katika ofisi ya Mwanasheria wa Serikali Kanda ya Arusha, lakini hakuna majibu ya uhakika waliowahi kupewa.

Mzee Motika anasema kwamba wamekuwa wakiambiwa kuwa faili limepelekwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

“Hata huko kwa DPP tumefuatilia lakini tumekuwa tunazungushwa, tumechoka na tunaomba watetea haki za binadamu waingilie kati mauaji ya watoto wetu waliouawa bila hatia,” alisema Mzee Motika wakati akizungumza na NIPASHE.

Motika alieleza kuwa inaonekana kwa nyakati hizi kwa mtu wa kawaida kupata haki ni jambo gumu sana kutokana na timu iliyoundwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima, kubaini na kuthibitisha kuwa vijana hao hawakuwa majambazi.

Alifafanua kuwa timu hiyo ilibaini pia kwamba halikuwepo hata tukio la ujambazi lililotokea katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara maarufu mwenye asilia ya Kiasia.

“Hatujamsahau kijana wetu, alikuwa sehemu ya maisha yetu, alikuwa na ndoto za maisha marefu, lakini yakakatizwa kinyama na polisi bila huruma,” alisema Mzee Motika na kuwa kibaya zaidi ni kuona jambo hilo likizimwa na wataalamu ambao yeye aliwaamini kuwa ni walinzi wa watu.


Alisema kuwa jambo baya zaidi ni kuwa watuhumiwa wa mauaji ya watoto wao wanaendelea kuwa huru huku wengine wakiwa wamepandishwa vyeo.

FAMILIA YA MAREHEMU MTUI

Kwa upande wa familia ya marehemu Mtui, wanadai kuwa hata baadhi ya  mali za marehemu Ewald zilipotelea polisi.

“Watoto wawili wa marehemu wanapata shida wameacha shule baada ya kukosa karo na mahitaji mengine muhimu,” alisema baba mzazi wa marehemu Mtui, Joseph Mtui.

Kuna taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwepo wakati huo wamepandishwa vyeo na kuhamishiwa vituo vipya vya kazi, wakiwemo ofisa upelelezi wa makosa ya jinai wakati huo.

Mmoja wao ni Leonard Paulo ambaye kwa sasa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa mpya wa Geita. 

Yumo pia aliyekuwa anakaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi wakati tukio hilo linatokea, Marko Kazumari, ambaye  amepandishwa cheo na kurudishwa Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dare es Salaam.

Taarifa nyingine kutoka kwa askari polisi mkoani hapa zimeeleza kuwa askari waliotekeleza mauaji hayo walihamishiwa vituo vipya vya kazi miaka miwili iliyopita.

“Unajua ile issue (suala) ilikuwa mbaya sana, lakini naona jamaa wamefanikiwa kusalimika na haya mambo yaliwahusu wakubwa wengine ambao kama wangeadhibiwa na wao wangeguswa,” alisema askari mmoja katika kituo kikuu wilayani Longido alikokuwa amehamishiwa mmoja wa watuhumiwa.

Akizungumza na NIPASHE, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema kuwa hajawahi kupokea malalamiko ya wazazi wa vijana hao tangu ahamie mkoani hapa  miezi mitano iliyopita.

Hata hivyo, Kamanda Sabas alihidi kufutilia suala hilo ingawa alionyesha wasiwasi kwa kuwa suala hilo liko katika mamlaka nyingine ambayo ni ofisi ya Mwanasheria wa Serikali.

Juhudi za NIPASHE kupata ufafanuzi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Arusha hazikuzaa matunda baada ya ofisa aliyedai kuwa yeye siyo msemaji kusema hakuwa na namba ya jalada lilo.

“Bosi yuko safari kikazi, kama ungenipatia namba ya jalada ningeweza kukusaidia kuangalia limefika wapi, lakini haiwezekani faili kama hilo kukaa kwetu muda mrefu, huenda lipo kwa DPP,” alisema ofisa huyo ambaye alikataa kutaja jina lake.

Machi Mosi mwaka 2009, polisi mkoani Arusha waliwaua kwa kuwapiga risasi Mtui (36) na Motika (22) na kutoa taarifa katika mkutano na waandishi wa habari kuwa waliwaua wakati wakipambana nao na kwamba walikuwa ni majambazi sugu waliokuwa wakitaka kupora katika kituo cha mafuta.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Ofisa Upepelelezi Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO), Leonard Paulo na aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Marko Kazumari.

Mkutano huo uliingia dosari baada ya viongozi hao kushindwa kujibu maswali ya waandishi wa habari kufuatia utata wa mazingira ya tukio hilo.

Baada ya hali hiyo kujitokeza, gazeti hili liliamua kufuatilia kwa kina kwa kuhoji watu walioshuhudia tukio hilo wakiwemo majirani wa kituo cha mafuta cha Gapco Kijenge na kuandika taarifa za tukio hilo.

Wiki moja baadaye, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati huo Isidore Shirima, aliunda kamati ya kuchunguza.

Kamati hiyo ilikuwa na uwakilishi kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi Makao Makuu, uwakilishi wa jamii na mwanasheria kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kamati ilifanya uchunguzi kwa wiki tatu na baadaye kutoa matokeo ya uchunguzi.

Shirima alitangaza na kuweka wazi kuwa kamati ilibaini kuwa halikuwepo tukio la ujambazi lililotokea katika kituo cha mafuta.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa vijana hao hawakuwa majambazi kwani hawakukutwa na silaha yeyote walipokamatwa na kuuawa wakiwa wamejisalimisha.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment