WAKATI vilio, simanzi na huzuni vikighubika jiji la Mwanza wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Barlow, mwanafunzi wa darasa la tano amedhalilishwa kingono na mtu asiyefahamika.
Mbali ya simanzi hizo, baadhi ya waombolezaji walianguka na kuzirai akiwemo mkewe, Marystella Barlow, aliyeishiwa nguvu ghafla katika tukio hilo ambalo lilihudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo viongozi wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Pia makamanda wa polisi wa mikoa yote sita ya Kanda ya Ziwa, walishiriki shughuli hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Nyamagana na baadaye jioni mwili kusafirishwa kwa ndege kwenda jijini Dar es Salaam ambapo familia ya marehemu inaishi.
Katika hatua ya kushangaza, mwanafunzi huyo wa shule moja jijini hapa, alijikuta akifanyiwa udhalilishaji wa kingono kwenye maungo yake sehemu ya makalio ambapo mwanaume mmoja asiyefahamika alimchafua sare yake kwa kumwagia manii pasipo kujua.
Tukio hilo la kufedhehesha kwa mwanafunzi huyo ambaye jina linahifadhiwa lilitokea wakati wananchi wakiwa wamebanana kwa ajili ya kushuhudia shughuli za kuagwa kwa mwili wa Barlow.
Mwanafunzi huyo alikuja kubaini tukio hilo la kuchafuliwa sare yake kwa manii baadaye, hivyo akaondolewa eneo hilo kwa msaada wa polisi.
“Nani amenimwagia maji huyo…jamani haya maji maji yametoka wapi?” alihoji mwanafunzi huyo baada ya kubaini tukio hilo kabla ya kuondolewa eneo hilo.
Hata hivyo hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio hilo lililozua minong’ono kwa waombolezaji huku baadhi yao wakilihusisha na matendo ya kishirikina.
Katika kuaga mwili huo, mke wa marehemu aliishiwa na nguvu na hivyo baadhi ya askari wa kike kumbeba na kumwingiza kwenye gari lililokuwa likitumiwa na Kamanda Barlow kwenye shughuli zake.
Akizungumza katika maombolezo hayo, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Robert Manumba, aliwahakikishia wananchi kuwa watuhumiwa waliohusika kwenye tukio la mauji hayo, watakamatwa wote ndani ya muda mfupi ujao.
Alisema kazi kubwa iliyokwishafanyika hadi sasa ya kuwasaka watuhumiwa ni kubwa lakini imefanikishwa kwa ushirikiano wa wananchi waliotoa taarifa mbalimbali.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alisema kuwa serikali imejipanga vyema kuhakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa na kamwe unyama wa aina hiyo hauwezi kuvumiliwa kwa raia yeyote.
Kamanda Barlow aliuawa usiku wa kuamkia Oktoba 13 majira ya kati ya saa saba na nane kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika eneo la Kitangiri wakati akimrudisha nyumbani Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyamagana, Doroth Moses.
Watu 15 akiwemo mwalimu huyo, wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi kuhusiana na kifo hicho ambacho kimezua utata mkubwa jijini hapa.
Marehemu Barlow alizaliwa Desemba 26, 1959 katika kijiji cha Kiyouu, wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, na kupata elimu sehemu tofauti nchini.
Ameacha mke na watoto watatu.
Chanzo:daima
No comments:
Post a Comment