Wednesday 7 November 2012

PINDA:MSIFARAKANE KWA SABABU YA DINI!!


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaasa Watanzania kutokubali kutenganishwa au kufarakanishwa kwa misingi ya kidini kwa sababu lengo la dini zote za Kiislam, Kikristo na Kimila ni kukuza ustawi, umoja na mshikamano ndani ya jamii husika.

Akizungumza na Jumuiya ya Wanataaluma, wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Mount Meru kilichoko eneo la Ngaramtoni, wilayani Arumeru juzi, Pinda alisema Watanzania wakikubali kutenda dhambi ya kutengana kwa imani ya dini zao, Taifa litaangamia kwa sababu uhasama wa kidini ni mbaya kuliko zote kutokana na kuhusisha imani.

“Dini na madehebu yote yanawaandaa waumini wake kuelekea njia sahihi ya kwenda peponi ambayo msingi wake ni upendo na kutenda haki kwa wote, kubaguana kwa misingi ya dini zetu ni kwenda kinyume cha maandiko matakatifu,” alisema Pinda

Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Taasisi ya elimu ya Baptisti na mahafali ya nane ya Chuo Kikuu cha Mount Meru, aliusifia uongozi wa chuo hicho kwa kutobagua wanafunzi katika misingi ya kidini licha ya kumilikiwa na taasisi ya kidini ya Kikristo.

Kauli ya Pinda inakuja huku Taifa likianza kushuhudia machafuko yanayochukua mkondo wa imani za kidini baada ya watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Sheikh Issa Ponda kuvamia na kuharibu makanisa eneo la Mbagala  Dar es Salaam baada ya kuchukizwa na kitendo cha mtoto mmoja kukojolea Qur’an Takatifu alipkuwa akibishana na mwenzake.

Wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho pia wamekuwa wakikabiliana na polisi katika matukio kadhaa  Zanzibar ambako pia makanisa , bar na majengo ya serikali yalivamiwa, kuharibiwa na kuchomwa moto.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baptisti Tanzania, Mchungaji Richard Mwaihuti amewataka wasomi nchini kutumia elimu yao kwa kutatua matatizo yanayoikabili jamii pindi wanapokabidhiwa madaraka ili
kuchochea maendeleo na ustawi wa umma.

“Wananchi wanahangaika kutafuta haki na huduma na wapo wataalamu waliokabidhiwa madaraka na jukumu la kuwahudumia na kuwapa haki hiyo, lakini hawafanyi hivyo kwa sababu ya kukumbatia vitendo vya ubadhirifu na ufisadi vinavyopigiwa kelele kila siku katika huduma za kijamii,” alisema Mchungaji Mwaihuti

Alisema elimu pekee siyo kigezo cha utumishi uliotukuka na uadilifu bali uaminifu, kutenda haki na kuheshimu utu ndio njia sahihi ya kusaidia jamii kupitia utumishi wa umma.
Zaidi ya wahitimu 570 walitunukiwa vyeti, diploma, shahada na stahahada
ya uzamili kwenye fani mbalimbali zikiwemo thiolojia, elimu na
maendeleo ya jamii.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment