UTAPELI wa aina yake, umeibuka mkoani Kilimanjaro ambapo kundi la matapeli hula njama na wanawake kuandaa mitego ya fumanizi na kujipatia mamilioni ya shilingi.
Uchunguzi wa kina wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa kundi hilo limekuwa likiwalenga wanaume walio katika ndoa na wenye uwezo wa kifedha, ambao baada ya kunaswa katika fumanizi hizo hupigwa picha zinazogeuzwa mradi.
Utapeli huo unawalenga wafanyabiashara, watu wenye nyadhifa kwenye taasisi na hata viongozi wa dini.
Kundi hilo lenye mtandao mpana nchini, linaonekana katika siku za karibuni kujikita katika mkoa wa Kilimanjaro.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa katika kipindi cha wiki mbili, watu wanne wamejikuta wakinaswa katika mtego huo na kutoa kitita cha kati ya Sh3 milioni na Sh10 milioni, gharama hizo zikiwa nje ya zile za kukomboa picha.
Kundi hilo hufanya kazi kwa kuwatumia wasichana wadogo na wakubwa, ambao wanaajiriwa maalumu kwa kazi hiyo ambayo haitofautiani na ya uchangudoa.
Mbali na waume za watu, wengine ambao wamenaswa kwenye mtego huo ni baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki, ambao hulazimika ‘kumalizana’ nao wakihofia kuchafuliwa kwa kashfa iwapo jambo hilo litaanikwa kwa umma.
Katika tukio la hivi karibuni, mfanyabiashara mmoja wa mjini Moshi alinaswa katika fumanizi hilo na mwanamke mmoja aliyedaiwa ni mkazi wa eneo la KDC Barabara Kuu ya Moshi-Himo na kulipa Sh3 milioni.
“Kwa hofu ya taarifa kumfikia mkewe, jamaa yangu aliamua kutoa fedha walizotaka, na unajua unapofumaniwa akili zinapotea kwa muda na unakuwa huna ujanja,” kilidokeza chanzo chetu.
Hata hivyo, chanzo hicho kilidai kuwa baada ya kupita wiki moja, mfanyabiashara huyo alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwandishi wa gazeti moja la udaku akimtaarifu kuwa ana picha za mfanyabiashara huyo alizopigwa kwenye fumanizi.
“Baada ya hapo tuliifuatilia namba yake na tumegundua anaitwa (jina tunalo), lakini kule kwenye lile gazeti hawamfahamu kabisa wala hiyo namba hawaijui,” alidai ndugu wa mfanyabiashara huyo.
Alidai kuwa, baada ya kumfuatilia mwanamke anayedaiwa kufumaniwa na ndugu yao, waligundua pia kwamba, tukio hilo ulikuwa ni mchezo mchafu.
Ndugu huyo alidai kuwa, mwanamke huyo anafahamika mjini Moshi na kwamba, anaishi kwa ujanja-ujanja kwani hana kazi maalumu na wala hajaolewa.
Kati ya matukio 10 yaliyotokea, tapeli huyo anayejifanya mwandishi wa gazeti hilo la udaku, ndiye anayetajwa kuhusika kupiga simu, akitishia kuwa asipolipwa, atachapisha picha za fumanizi.
Imedaiwa kuwa, vigogo wenye nyadhifa mbalimbali katika taasisi kadhaa mkoani Kilimanjaro wameingia kwenye mtego huo.
Padri mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa, pia anadaiwa kunaswa katika mtego huo na kulipa Sh5 milioni, lakini baadaye alilazimika kutoa kitita kingine cha Sh3 milioni ili kukomboa picha zake.
Uchunguzi umebaini kuwa padri mwingine wa shirika moja alilazimika kutoa Sh6 milioni, baada ya ‘mwandishi’ huyo kumpigia simu akimweleza ana picha za mtoto aliyezaa na mwanamke mmoja.
“Unajua hawa wenzetu hawaruhusiwi kufanya tendo la ndoa, lakini baadhi yao tunaowafahamu wana watoto, hivyo wanapotokewa huwa wanachanganyikiwa,” alidokeza ndugu wa karibu wa padri huyo.
Hata hivyo, baadhi ya wanawake waliohojiwa na gazeti hili walidai kuwa wako tayari kukilipa kikundi hicho ili waume zao wafumaniwe na kuaibishwa kama njia ya kuwarejesha kwenye mstari.
Pamoja na kukiri kuwapo kwa mchezo huo mkoani humo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema uhalifu huo ni vigumu kuudhibiti kwa vile wanaofanyiwa hivyo hawawezi kutoa taarifa polisi wakihofia wake zao kubaini uchafu wao.
Alisema kuwa, badala ya waathirika wa matukio hayo kuwafichua wahusika wa matukio hayo, huamua kufa na tai shingoni huku wakiendelea kugeuzwa mradi na matapeli hao na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kikundi hicho cha matapeli kiweze kukamatwa.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment