Friday 25 January 2013

JK amponza ofisa usalama


MTU mmoja anayedaiwa kuwa ni ofisa usalama wa taifa, amenusurika kuuawa na wananchi wa kijiji cha Msimbati, kata ya Madimba, wilayani Mtwara, akidaiwa kutumia jina la Rais Jakaya Kikwete kutaka kumrubuni mkuu wa kaya ya Wasimbati abadili msimamo wake kwenye sakata la gesi.
Hivi karibuni mkuu huyo wa Wasimbati, Somoe Mtiti (106), aliionya serikali kuwa endapo italazimisha kusafirisha gesi kutoka Mtwara bila maridhiano na wananchi, ingelifika Dar es Salaam ikiwa maji.
Kwa mujibu wa mwandishi wetu aliyefika kijijini hapo jana kufuatilia tukio hilo, shangazi wa mtuhumiwa, Fatuma Tom, alikiri kijana wake Seleman Babu kufika kijini hapo juzi saa 10 alasiri na kumwomba ampeleke kwa bibi yule mkuu wa kaya.
Fatuma alisema kuwa kijana wake Babu ni ofisa usalama wa taifa anayefanya kazi jijini Dar es Salaam na kwamba alimsindikiza hadi kwa bibi huyo ambapo baada ya kufika, alimweleza kuwa ametumwa kwake na viongozi wa juu aondoke naye kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo na Rais Kikwete na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia.
Fatuma alisema kuwa bibi yule alikataa maelezo hayo licha ya Babu kumshawishi sana akisema kama hawezi kuondoka wakati huo kuna gari ingelimpitia Jumanne ijayo.
“Kadiri mabishano yalivyozidi walinzi wa bibi waliingilia kati huku wananchi wakizidi kukusanyika na hivyo kumtaka kijana wangu aondoke, lakini akawa anabisha,” alisema.
Kadiri watu walivyoongezeka, hali ilibadilika na kuanza kumrushia mawe kijana yule aliyekimbilia kwenye gari lake lenye namba za usajili T609 PXG aina ya Mark II na kuondoka kwa kasi, lakini kwa kuwa ni mgeni na njia alijikuta akikwama, hivyo kufungua mlango na kutimua mbio.
Shangazi huyo aliongeza kuwa wananchi waliendelea kuliponda gari hilo kwa mawe kisha kuliteketeza kwa moto wakiwa wamekasirishwa na hatua hiyo ya kijana huyo wakitafsiri kuwa ni mpango wa serikali kutaka kumuua mkuu wao wa kaya ili wafanikishe malengo yao ya kupeleka gesi Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Salum Athuman, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba gari alilokuwa akitumia Babu, ni mali ya mdogo wake Mussa Babu kwa mujibu wa vielelezo walivyovikuta ndani ya gari hilo.
kushuhudia masalia ya gari hilo, Babu alipotafutwa kwa simu, alikana kushambuliwa akidai hajawahi kwenda huko siku za karibuni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki, alisema kuwa Babu hajaenda polisi kulalamika hivyo hawana taarifa za kushambuliwa kwake.
Bibi Somoe amekuwa maarufu sana kijijini hapo kiasa cha uongozi kumwekea ulinzi kutokana na uwezo aliouonesha mwaka 2005 wakati wa uchimbaji wa gesi, alipoitwa na makampuni kuyasaidia baada ya mitambo yao kugoma kushuka chini wala kupanda juu.
Inaelezwa kuwa baada ya bibi huyo kufanya tambiko katika mitambo hiyo ndipo ikaanza kufanya kazi yake kama kawaida, hivyo tishio lake kwa serikali kuhusu sakata la gesi linaloendelea liliwatisha viongozi wa serikali.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment