Monday 28 January 2013

Kikwete rudi umalize ugomvi wa gesi Mtwara


MZOZO wa gesi mkoani Mtwara umefika mahali pabaya na serikali lazima ielekeze nguvu zake huko kuhakikisha mzozo huo unamalizika.
Kwa takriban wiki mbili sasa, vyombo vingi vya habari vimekuwa vikiripoti taarifa mbalimbali kueleza jinsi wananchi wa Mtwara wasivyoridhika na uamuzi wa serikali kujenga bomba la gesi kutoka mkoani humo kuja jijini Dar es Salaam bila kuwaambia wao watanufaika vipi.
Mengi yameandikwa na p engine serikali haikuona uzito, lakini baada ya tukio la jana, tunadhani ni wakati muafaka sasa kuamka na kulishughulikia jambo hili ili kurejesha amani Mtwara.
Hatuna nia ya kurejea kila kitu kilichotokea kwenye vurugu za jana, lakini kwa kifupi ni kwamba nyumba, magari na mali nyingine za wabunge, Anna Abdallah (Viti Maalumu) na Mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe, wote wa CCM, zimeteketezwa kwa moto na baadhi ya wananchi.
Wabunge hao wamekumbwa na mkasa huo kwa madai kuwa ni wasaliti, eti wameungana na serikali ya Rais Kikwete kuwahujumu juu ya gesi yao.
Uharibifu mwingine uliofanywa katika vurugu hizo ni pamoja na kuchoma majengo ya serikali, vituo vya Polisi na kusababisha vifo vya watu wanne, akiwemo askari polisi mmoja.

Itoshe tu kusema kwa kifupi kwamba hali ya amani katika Mkoa wa Lindi na Mtwara iko shakani na serikali isipokuwa makini, maafa na madhara makubwa zaidi yanaweza kutokea.
Lakini haya yote yakitokea, Rais Jakaya Kikwete yuko ziarani nje ya nchi. Tunajua rais yuko kwenye ziara muhimu ya kikazi, lakini katika hili tunamsihi akatishe ziara hiyo ili apate fursa ya kushughulikia mzozo huo.
Tunajua urais ni taasisi, lakini mambo makubwa kama hayo yakitokea katika nchi na rais akiwa hayupo, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Lakini upande wa pili wa shilingi, sisi tunadhani serikali ilipaswa kutoa elimu ya kutosha kabla ya mradi huo kuanza.
Ukizungumza na baadhi ya wakazi wa mikoa hiyo kwamba, kwanini wanapinga, hawana sababu za msingi, ni kama wanafuata upepo, hivyo wanahitaji elimu zaidi kujua faida ya mradi huo.
Jambo jingine kubwa kuliko yote, serikali inapaswa kuwasaka wote walio nyuma ya vurugu hizi, hata mataifa ya nje, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuwapo msukumo kutoka nchi hizo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment