Sunday, 13 January 2013

Mama aua mwanae, amnyofoa viungo


MTOTO wa miezi 11, Happy Antony, mkazi wa Kitongoji cha Mwangaza, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, ameuawa kikatili na kunyofolewa viungo vyake vya mwili na mama yake mzazi, kisha kutoweka navyo kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Tarime na Rorya, Justus Kamugisha, aliliambia Tanzania Daima Jumapili ofisini kwake jana kuwa, tukio hilo lilitokea majira ya saa 2.00 asubuhi baada ya mama huyo, Prischal Mwita (22) kudaiwa kumuua na kumnyofoa viungo vyake vya mwili mtoto wake kwa imani za kishrikina.
Kamugisha alivitaja viungo vilivyobainika kunyofolewa baada ya marehemu huyo kufanyiwa uchunguzi na daktari wa hospitali ya wilaya kuwa ni sikio, nyusi za macho, ngozi na nywele zake za kichwa.
“Mama huyo amefanya tukio la ajabu, amemuua mwanae wa miezi 11 na kisha kumnyofoa viungo vyake vya kushoto na kisha kutoweka navyo, tunadhani ni mauaji ya kishirikina, mama huyo tumemkamata na tunaendelea kumhoji juu ya tukio hilo, lakini hasemi chochote kile,” alisema Kamanda Kamugisha.
Alisema kuwa taarifa za kuwepo kwa mauaji hayo ya kinyama na kishirikina katika eneo hilo zilitolewa kwa Jeshi la Polisi na mwenyekiti wa kitongoji hicho, Nchama Makaranga.
Kamugisha alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini wahusika wengine wa tukio hilo, huku wakimshikilia mama wa mtoto huyo na baadae kumpandisha kizimbani wakati wowote ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alitengana na mumewe muda mrefu, aliyefahamika kwa jina la Mwita Antony.
Tukio kama hilo liliwahi kutokea miaka michache iliyopita ambapo mwanamme mmoja aliuawa na  kisha kunyofolewa ngozi ya mwili wake na kukatwa katwa vipande vipande na kutunzwa kwenye gunia katika mji mdogo wa Sirari.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment