Friday, 11 January 2013

Mshtakiwa: Najua siri nyingi za Mwinyi


MTUHUMIWA anayedaiwa kumuibia rais mstaafu All Hassan Mwinyi sh.milioni 37, Abdallah Nassor Mzombe (40) zikiwa ni kodi ya pango katika nyumba mbili zinazomilikiwa na rais huyo, ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa anajua siri nyingi za Mwinyi ambazo kamwe hawezi kuzisema mahakamani hapo.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Jenevitus Dudu, katika utetezi wake, mbali ya kukataa kutenda kosa hilo, Mzombe alidai amefanya kazi nyingi na kushirikishwa na mzee Mwinyi mambo mengi ya wazi na ya siri ambayo hata watoto wake wa kuzaa hawayajui na kwamba anashangazwa kuona sasa anashtakiwa kwa makosa ya kumuibia fedha hizo.
Mzombe ambaye wakati akitoa utetezi wake alikuwa akiangua kilio na kulitaja jina la Mungu, alidai ameanza kufanya kazi za Mwinyi tangu mwaka 1996 na kwamba Mwinyi amekuwa akimuamini.
Alidai kuwa hakukuwa analipwa mshahara maalumu na Mwinyi kwani alimchukulia kama mwanae.
“Mzee Mwinyi aliniamini sana na hata mambo mengine ambayo amekuwa akituma nifanye siwezi kuyasema hapa mahakamani, kwani hata watoto wake hakuwahi kuwashirikisha…hizo nyumba mbili mnazodai mimi nimemuibia fedha si kweli, kwani Mzee Mwinyi amekuwa akinipa zaidi ya shilingi milioni 300 bila kuandikishiana sehemu niende nikamnunulie nyumba, mashamba, nikamjengee majumba na nimekuwa nikifanya hivyo na kuandika jina lake.

“Mwendesha Mashtaka naomba nikuulize, unaujua uhusiano wetu na Mwinyi? usitake niseme mengi hapa..hivi unafahamu kuwa nilishakaa na Mwinyi tukajifungia na kuongea na kukubaliana kwamba ninavyomfanyia shughuli zake hizo kwa uaminifu tena bila hata watoto wake hawajui ipo siku ataninunulia nyumba? lakini hadi leo nyumba hajaninunulia,” alidai.
“Mheshimiwa hakimu, mimi sina crown, sina fedha na hao wapangaji waliokuja kutoa ushahidi kuwa walinipa kodi mimi sikumpelekea Mwinyi ni waongo na sijawahi kugombana nao isipokuwa mpangaji mmoja ambaye tangu mwanzo nilimuona kama ni mkorofi.
“Kwa kuwa Mwinyi ni kiongozi mkubwa ni wazi mashahidi hao wanaweza wakawa walishinikizwa kuja kutoa ushahidi wa kunikandamiza, ila nasema sina madaraka, fedha na mashahidi ambao nilikuwa nategemea waje kunitolea ushahidi wananipiga chenga kwa sababu wapo karibu na Mzee Mwinyi….kikubwa hapa naomba mahakama initendee haki,” alidai Mzombe huku akiangua kilio.
Kuhusu wizi wa fedha za kodi nyumba hizo za Mikocheni na Msasani, Mzombe alidai kushangazwa na tuhuma hizo, kwani ni rais Mwinyi ndiye aliyempa fedha za kwenda kumnunulia nyumba hizo na alikuwa akizisimamia wakati wa kufanyiwa ukarabati.
Bada ya kumaliza utetezi huo, Hakimu Dudu alisema hukumu ya kesi hiyo ataitoa Februari 12 mwaka huu.
Oktoba 9 mwaka jana, rais All Hassan Mwinyi alifika mbele ya Hakimu Dudu na kutoa ushahidi wake, lakini hata hivyo wana usalama ambao walikuwa wakimlinda waliwazuia waandishi wa habari kuingia mahakamani kusikiliza ushahidi huo.
Katika kesi hiyo, Mzombe anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai mwaka 2012 huko Mikocheni, akiwa Wakala wa rais huyo alimwibia sh milioni 17 ambazo ni pato la kodi ya nyumba yake iliyopo eneo la Mikocheni.
Aidha, alidai kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 10, mwaka huu huko Msasani Village, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alimwibia rais huyo sh. milioni 19.8 ambayo ilikuwa ni kodi ya nyumba namba 55 iliyopo kwenye Kitalu C.

No comments:

Post a Comment