RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutokana na kifo cha msanii maarufu hapa nchini, Juma Kilowoko ‘Sajuki’, kilichotokea usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na kifo cha msanii Juma Kilowoko, ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha sanaa, hususan michezo ya kuigiza na filamu hapa nchini. Kwa hakika kifo cha msanii huyu ni pigo kubwa kwa tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu, ambayo inaendelea kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake hizo za rambirambi.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakuomba wewe Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara, unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Juma Kilowoko kwa kuondokewa na kiongozi na baba wa familia.
“Natambua uchungu iliyonao familia ya marehemu Kilowoko, lakini nawahakikishia kwamba, binafsi niko pamoja nao katika kuomboleza kifo cha mpendwa wao. Nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu Juma Kilowoko, amina,” alisema Rais Kikwete.
Nalo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limeelezea kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Sajuki.
“Baraza limeshtushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Sajuki, ambaye mchango wake unahitajika sana katika tasnia ya sanaa, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wao bado unahitajika katika tasnia hii,” alisema Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche Materego.
Aliongeza kuwa, baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, na linawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.
Sajuki ni mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma na alianza kujihusisha na masuala ya maigizo alipojiunga na kikundi cha Kaole na baadaye kuingia katika filamu. Filamu alizocheza ni pamoja na ‘Revenge’ ya Kampuni ya RJ.
Mwaka 2008, aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe, ambapo filamu yake ya kwanza ilikuwa ni ‘Two Brothers’ kwa kushirikiana na Shija Deogratious. Baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo Wajey Production, ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo ‘Mboni Yangu’, ‘Round’, ‘Briefcase’, ‘Kijacho’, ‘Kozopata’, ‘Mchanga na Keni’, ‘077’ nk.
Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011, ambapo alikwenda kutibiwa nchini India.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment