Sunday 27 January 2013

Wanafunzi wa kike wakumbwa na ugonjwa wa ajabu


Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya De Paul inayomilikiwa na Kanisa la Katoliki jimbo kuu la Mbinga mkoani Ruvuma wamekumbwa na ugonjwa wa ajabu wa kuweweseka na kupooza viungo.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwenye shule hiyo zimesema kuwa siku tatu zilizopita dalili zilianza kuonekana kwa baadhi ya wanafunzi ambao baadae hali zao ziliendelea kuwa mbaya na uongozi wa shule ulilazimika kuwakimbiza kwenye hospitali kwa matibabu.
Wanafunzi tisa walikumbwa na ugonjwa huo wa kuweweseka na kupooza baadhi ya viungo vya miili yao.
Habari zaidi ambazo zimeelezwa na baadhi ya wanafunzi na walimu ambao wameomba majina yao yahifadhiwe, zilisema kuwa siku ya pili wanafunzi wengine saba walibainika kuwa na tatizo hilo na kupelekwa katika hospitali ya serikali ya wilaya kwa matibabu.
Jitihada za kuupata uongozi wa shule hiyo ziligonga mwamba baada ya kutopatikana kwa simu zao za mikononi.
NIPASHE ilimpata Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Dk. Damas Kayela, ambaye alikiri kuwapokea wanafunzi 16.
Dk. Kayela alisema kuwa baada ya kuwapokea wagonjwa hao, jopo la madaktari lilianza kuwahudumia kwa kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na matatizo yaliyokuwa yanawakabiri lakini baadae jopo la madaktari lililazimika kwenda kwenye eneo la shule ya De Paul ambapo walipofika waliwakuta wanafunzi wengine sita wakiwa wanasumbuliwa na tatizo hilo. Baadaye iligundulika kuwa tatizo lililowakumba wanafunzi hao ni la ugonjwa wa kuchanganyikiwa na kulegea mwili.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga, alithibitisha kuwa wanafunzi 22 wa shule hiyo waligungulika kuwa na ugonjwa wa kuchanganyikiwa na kulegea mwili na kwamba kwa sasa wataalamu wa afya wakiwemo madaktari walishakwenda kwenye shule hiyo kutoa ushauri zaidi kwa wanafunzi na uongozi wa shule hiyo.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment