Thursday 16 May 2013

Ajiua akidhani ameua mwanae kwa kumchoma kisu shingoni


MKAZI wa Kivule, Dar es Salaam, Emmanuel Salagata (45-50) amejiua kwa kujinyonga baada ya kumchoma kisu shingoni mwanae.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minagi, alisema jana Salagata alijinyonga juzi, majira ya saa 2 asubuhi maeneo ya Kitunda kwa kutumia kamba aliyokuwa ameitundika kwenye dari chumbani kwake.
Alisema siku moja kabla ya tukio, Salagata akiwa kwenye kilabu ya pombe kwa Mama Zawadi, alimchoma kisu shingoni mwanaye George Emmanuel (30) ambaye alitibiwa katika Hospitali ya Amana na kuruhusiwa.
Kamanda Minagi alisema sababu za mzazi huyo kumchoma mwanaye kisu ni katika hali ya ulevi na alipoona hivyo alijua amemuua mwanaye ndipo alipoamua kujinyonga.
Kwa mujibu wa Minagi, marehemu aliacha ujumbe unaosomeka: “Nimejiua kwa kujinyonga kwa amri yangu na kero za watu”. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakati huohuo, fundi ujenzi, Peter Salum (40) amekutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya manila aliyoitundika kwenye kenchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12:00 jioni maeneo ya Kimara Mavurunza.
Sababu za kujinyonga bado hazijafahamika kwa kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment