Tuesday 21 May 2013

POLISI AMCHARANGA MAPANGA MWANAYE KISA MAPENZI



KATI ya stori za mwaka zinazosikitisha, hii ni mojawapo! Polisi mstaafu, mkazi wa Kitongoji cha Sango, Kata ya Nyasubi wilayani Kahama mkoani hapa, Samson Bwire (54), anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kumcharanga mapanga binti yake, Devotha Gerald (4), kisa kikidaiwa ni wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo lilitokea Mei 16, mwaka huu, majira ya jioni nyumbani kwa Bwire alipokuwa akigombana na mke wake, Happiness Elias (28).
Kwa mujibu wa mashuhuda, baba Devotha anadaiwa kufanya tukio hilo huku akiwa amelewa tilalila.
Habari zilidai kuwa, mwanaume huyo alikuwa kwenye ugomvi wa kimapenzi na mkewe ambapo katika purukushani akimtuhumu mama Devotha kumsaliti, mkewe huyo alifanikiwa kuchoropoka.
Ilidaiwa kuwa baada ya mama Devotha kuchoropoka ndipo baba huyo akamgeuzia kibao Devotha na kumalizia hasira zake kwa kuanza kumkatakata kwa panga bila huruma.
Kwa mujibu wa majirani, kelele zilisikika kutoka kwenye familia hiyo na kwamba walipokwenda walimkuta baba Devotha akichoma nguo za mkewe na alipowaona, aliingia ndani na kuanza kumkata mapanga mtoto huyo huku akiwa amefunga mlango.
Ilifafanuliwa kwamba baada ya kusikia kelele za mtoto, majirani walianza kuvunja mlango huku wakiomba msaada kutoka kwa polisi na baada ya polisi kufika walifanikiwa kumnusuru mtoto akiwa amejeruhiwa vibaya.
Kufuatia hali mbaya ya mtoto aliyekuwa amelowa damu kichwani, majirani walishindwa kuzuia hasira zao na ndipo walipoanza kumpiga Bwire ambaye ni askari polisi mstaafu wa cheo cha koplo.
Katika hali kama hiyo, ilibidi polisi wafanye kazi ya ziada kumnusuru baba Devotha na kumpakia kwenye gari kwenda kituoni.
Hata hivyo, wakati gari la polisi likiwa katika mwendo wa kasi eneo la Soko la Mkulima, baba Devotha aliruka kutoka kwenye gari na kuangukia lami, kitendo kilichomsababishia majeraha makubwa sehemu za usoni.
Mtoto Devotha na baba yake, wote walikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu huku Bwire akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ikiwa ni pamoja na kufungwa pingu.
chanzo:globalpublishers

No comments:

Post a Comment