Wednesday 22 May 2013

Sakata la Jaydee, Clouds latua bungeni


MSEMAJI wa kambi rasmi ya upinzani, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (CHADEMA), amefikisha rasmi bungeni mgogoro kati ya mwanamuziki maarufu Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ na wamiliki wa Clouds Media.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo bungeni jana, Sugu alisema kuwa mgogoro huo umesababisha kutopigwa nyimbo za Bongo fleva kwa siku nzima.
Sugu alisema kuwa kwa sasa watu wachache wenye fedha wamewageuza wasanii kuwa ni sehemu ya mtaji wao, kwa kutumia sanaa zao kujitajirisha.
“Sanaa inaendelea kufanywa mtaji wa biashara wa watu wachache ambao wanatumia nguvu waliyonayo katika jamii na uwezo wao wa kifedha, katika kukandamiza maslahi ya wasanii hapa nchini,” alisema Sugu.

Alisema imebainika kuwa upo wizi wa kutisha kwa wasanii kuibiwa kazi zao.
“Kutokana na hali hiyo, mimi binafsi pamoja na baadhi ya wasanii wachache, tulianzisha harakati za kudai haki kwa kupitia programu maarufu ya Ant Virus chini ya Vinega.
Lengo kubwa la kuanzisha programu hiyo, ni pamoja na kuhakikisha haki ya wasanii inadaiwa dhidi ya ukandamizaji unaofanywa na wajanja wachache kwenye muziki, ambao wanatumia nafasi yao kama njia ya kutumia mitaji yao ya fedha kuwaendesha wasanii jinsi wanavyotaka wao,” alisema Sugu.
Sugu ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, alisema kuwa wasanii wamekuwa na tabia ya kutokuwa na umoja na mshikamano, ndiyo maana kuna mgogoro unaofukuta na kusababisha msanii maarufu nchini Lady Jaydee kutopigwa nyimbo zake Redio Clouds kwa siku nzima.
Alisema kuwa mbali na kuwa umoja wa wasanii hasa wa kizazi kipya unasimamiwa na chombo halali kinachojulikana kama Tuma-‘Tanzania Urban Music Association’, kutokana na ujanja wa watu wachache, wameudhoofisha.
Aliongeza kuwa wajanja hao walianza kwa kuanzisha kampuni iliyosajiliwa kama Tanzania Flavors Unit (TFU), ambayo iliwaghiribu wasanii kwa madai kuwa ni muungano wa wana muziki wa Bongofleva na kuhodhi majukumu ya Tuma, ambacho ni chama halali cha kusimamia wanamuziki wa Bongofleva.
“Mpaka tunapoongea leo hii, hata studio iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete, bado iko katika mikono ya TFU pamoja na serikali kuamuru irudishwe katika mikono ya serikali ili ikabidhiwe kwa wasanii wote chini ya usimamizi wa chama halali cha Tuma,” alisema Sugu.
Aidha alisema kuwa wasanii nchini wanaendelea kuishi katika maisha magumu huku serikali ya CCM ikiendelea kuwapa maneno ya kashfa.
“Serikali acheni tabia ya kutatua migogoro kisiasa na badala yake tafuteni ufumbuzi wa kweli pale inapotokea migogoro kati ya wasanii na baadhi ya watu ambao ni wajanja wanaowatumia wasanii kama mtaji wao,” alisisitiza.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment