Monday 13 May 2013

Tusijidanganye kuzima udini bila kubaini chimbuko


MATUKIO mfululizo yanayoashiria uvunjifu wa amani yametuzindua usingizini na sasa kila mmoja hususani viongozi wetu wanaimba wimbo unaofanana wa kuwataka wananchi wadumishe amani.
Mlipuko uliotokea hivi karibuni katika Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti jijini Arusha wakati ibada ikiendelea, na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa, umeandika taswira mbaya kwa taifa.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache duniani yanayosifika kwa amani na utulivu. Kutokana na sifa hiyo, nchi nyingi za Kiafrika zilitegemea mchango wake wakati wa ukombozi.
Lakini matukio ya vurugu za kidini yaliyojitokeza kwenye maeneo mengi nchini na kusababisha majeruhi pamoja na vifo kwa baadhi ya viongozi wa kiroho, yameitia doa Tanzania.
Sasa viongozi wetu wanahaha kuzima matukio hayo kwa kujaribu kuchukua hatua kadhaa za kuwadhibiti wachochezi wa vitendo hivyo.
Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo ya kujaribu kurejesha heshima ya taifa letu machoni mwa mataifa, bado tuna kila sababu ya kubaini chimbuko la vitendo hivyo badala ya kujidanganya kuzima.

Muasisi wa taifa hili, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliona madhara ya chokochoko hizi za udini, hivyo kwa kushirikiana na wenzake wakaweka misingi ya kulifanya taifa lisifungamane na dhehebu lolote.
Kwa sababu ya siasa zetu zisizo na tija, wanasiasa wetu wamekubali kuwatumia baadhi ya viongozi wa dini kufanikisha malengo yao ya kisiasa huku wakiliacha taifa limegawanyika vipande.
Waliofanya haya wanajulikana, lakini walifumbiwa macho wakati wakifanya uchochezi huo. Halafu leo wale wale wanaibuka na kujiliza wakiwakemea wengine wajiepushe na matendo yanayoashiria uchochezi.
Kwa mantiki hiyo, tunaona ni vigumu kumaliza tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu ikiwa hatutaki kujielekeza kwanza kutafuta kiini chake.
Taifa limegawika vipande, wananchi hawana uhakika na usalama wao. Hivyo ni vigumu kuzima viashiria hivi kwa kauli laini badala ya kujielekeza kwanza kutafuta chanzo na kukitokomeza.
Tunaweza kuwakamata wale wote tunaowahisi kuwa wachochezi na kuwachukulia hatua za kisheria, lakini bila kutafiti kujua nani anafadhili mkakati huo na kwa malengo gani, tutakuwa tunafanya kazi bure.
Lazima tukubali kuwa kuna mahala tumeteleza, hatupaswi kunyanyuka na kuanza kutembea kuelekea mbele bila kuangalia ni kwanini tulijikwaa na kuanguka.
Kama tuliweza kudumisha amani yetu kwa miaka yote tangu uhuru, ni kwanini tukubali leo kuyumbishwa na kikundi kidogo cha watu wenye maslahi binafsi?
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment