Friday 31 May 2013

Uraia wawatesa Watanzania ughaibuni

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Watanzania wengi walio ughaibuni wanaathirika sana na suala la uraia wa nchi mbili.
Membe alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014, ambapo alibainisha kutokuwepo kwa sheria inayoruhusu uraia wa nchi mbili kunawafanya wakose ajira za kueleweka, huduma za afya, elimu na mikopo.
Membe alisema kuwa wizara hiyo katika maoni yake kwa Tume ya Katiba ililipa suala la uraia pacha kipaumbele kwa kuwa wanaamini kwamba kufanya hivyo kutawawezesha Watanzania walioko nje kuchangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya nchi.
Kuhusu ziara za viongozi wakuu wa kimataifa kuitembelea Tanzania, Membe alisema kuwa zimefungua milango mipya ya mashirikiano kati yake na mataifa pamoja na kuchochea na kukuza biashara.
Mbali na Rais wa Marekani ambaye anatarajiwa kuitembelea Tanzania hivi karibuni, Membe alisema kuwa vilevile kati ya Juni na Julai mwaka huu, Rais wa Sri-Lanka, Mahinda Rajapaksa, na Waziri Mkuu wa Thailand, Yungluck Shinawatra, watafanya ziara rasmi hapa nchni.
Nayo Kamati ya Mambo ya Nje katika maoni yake, ilisema kuwa licha ya wizara kukubali manufaa ya kutekeleza ushauri uliotolewa bungeni mwaka jana, mambo mengi hayakufanyiwa kazi kabisa.

“Kwa mfano, kamati ilishauri kuhusu kufanyika kwa mikutano ya mabalozi ili kufanya tathmini na kuboresha masuala mbalimbali ya utekelezaji balozini.
“Taarifa za wizara zilionyesha kuwa kwa mara ya mwisho mkutano wa mabalozi Tanzania ulifanyika Zanzibar mwaka 2008. Ni takriban miaka mitano sasa mikutano hiyo haijafanyika, jambo ambalo si jema,” alisema Juma Nkamia kwa niaba ya kamati.
Aliongeza kuwa kutokana na maelezo hayo ya matumizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ni dhahiri kuwa hali ya majengo ya balozi zetu nyingi inaachwa kuendelea kuwa mbaya na mengine kiasi cha kutisha.
“Kwa mfano, jengo la ofisi ya ubalozi wetu huko Brussels Ubelgiji lililonunuliwa mwaka 2004 kwa gharama ya euro milioni 1.5, limechakaa na kuvuja kiasi cha kusababisha baadhi ya kuta kutoa harufu mbaya na kuiaibisha nchini yetu,” alisema.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment