Friday 24 May 2013

Yule mtoto aliyecharangwa mapanga na baba yake afariki



                                          Devotha Gerald enzi ya uhai wake 
                                                Mama yake marehemu devotha
YULE mtoto wa miaka minne, Devotha Gerald aliyecharangwa mapanga kikatili na baba yake mzazi na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kwa matibabu, ameaga dunia.
Samson Bwire mkazi wa Kitongoji cha Sango, Kata ya Nyasubi, Wilayani Kahama mkoani hapa ndiye baba mzazi anayedaiwa kutenda unyama huo uliopitiliza.
Uhai wa Devotha ulikatika Mei 16, mwaka huu saa nne usiku akiwa amezungukwa na jopo la madaktari waliokuwa wakiupigania uhai wake.
Habari za kitabibu kutoka hospitalini hapo zinasema binti huyo aliaga dunia kutokana na kutokwa damu nyingi ambapo pia mapanga aliyokatwa yalizama kichwani.
Baadhi ya madaktari waliokuwa wakimtibu walitokwa machozi wakati mtoto huyo akikata roho. 
Mei 16, mwaka huu, majira ya jioni, Bwire ambaye ni polisi mstaafu alidaiwa kumcharanga mapanga mtoto wake huyo kisa kikidaiwa ni ugomvi uliotokana na wivu wa kimapenzi kati yake na mkewe, Happiness Elias (28).
Kwa mujibu wa mashuhuda, Bwire anadaiwa kufanya tukio hilo akiwa amelewa chakari. 
Habari zinadai kuwa, katika ugomvi huo, mwanaume huyo alikuwa akimtuhumu mkewe kumsaliti. Hata hivyo, mkewe alifanikiwa kukimbia kusikojulikana.
Baada ya mkewe kukimbia ndipo baba mzazi huyo akamgeuzia kibao mwanaye na kumkata mapanga kumaliza hasira zake.
Majirani walivunja mlango, wengine walipiga simu polisi ambao walifika na kumkamata mtuhumiwa.
Hata hivyo, Bwire hakuachwa salama kwani majirani hao wakiwa na hasira walimpiga sana.
Wakati mtuhumiwa akipelekwa polisi aliruka kutoka garini na kuangukia uso kitendo kilichomsababishia majeraha makubwa usoni.
Marehemu Devotha alizikwa Mei 17, mwaka huu mjini Shinyanga. Mama wa marehemu akizungumza kwa uchungu alisema: Maskini mwanangu amekufa kifo kibaya sana, wala hakuwa na hatia yoyote, naumia sana moyoni mwangu.
“Madaktari walipambana kuokoa uhai wake lakini Mungu akasema mwancheni aje kupumzika.”
chanzo:globalpublishers.

No comments:

Post a Comment