Thursday, 11 July 2013

Aliyefariki siku ya harusi azikwa na mwanaye


                                       Bi Levina Swai  enzi ya uhai wake

Rombo. Ilikuwa ni majonzi, vilio na huzuni katika kijiji cha Mahalu, wilayani Rombo, Kilimanjaro kufuatia mazishi ya aliyetarajiwa kufunga ndoa Jumamosi marehemu Levina Swai pamoja na mwanawe.
Marehemu Levina alizikwa na mwanaye kaburi moja baada ya kichanga hicho kufariki siku hiyo hiyo mara baada ya mama yake kupoteza maisha kwa kile kilichodaiwa ni kuugua Malaria, shinikizo la damu kuwa chini na upungufu wa damu.
Marehemu Levina alifariki wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza katika kijiji cha Mahalu kata ya Makiidiwilayani Rombo, alikozikwa,wifi wa marehemu, Hortensia Mrima alisema wifi yake alifia hospitalini na alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi akiwa katika mpango wa ajira ya walimu wapya.
“Mimi ndiye nilikuwa namuuguuza hospitalini tangu Alhamisi iliyopita na alikuwa anasumbuliwa na malaria na kupungukiwa na damu na pressure (shinikizo la damu) kuwa chini,”alisema Mrima.
Ibada ya mazishi ilianza saa 8:30 mchana ikiongozwa na Padri Emmanuel Mavengero na kuhudhuriwa na waombolezaji kutoka Tanga na Kilimanjaro.
Mazishi hayo yalitawaliwa na simanzi huku waombolezaji wengi akiwamo aliyetarajiwa kumuoa marehemu Levina,Gabriel Swai muda wote alikuwa akibubujikwa na machozi na kushindwa kuzungumza.
Wifi huyo alieleza kuwa wifi yake alipopimwa alikutwa na Malaria 13 na kupewa dawa za malaria za SP na dripu za Quinine ambazo zilimlewesha sana na kuendelea kudhoofu.
“Siku hiyo ya Alhamisi alikata kauli akawa haongei ikabidi daktari amwekee dripu za Glucose ili kumuongezea nguvu na shinikizo la damu ilirudi sawasawa lakini bado alikuwa amelegea na alikuwa haongei,”alisema.
Ilipofika Jumamosi ambayo ndiyo siku iliyokuwa imepangwa kufunga ndoa na Gabriel Swai, ikabidi madaktari wamuwekee maji ya uchungu ili kumuokoa mtoto baada ya mama kuwa mahututi.
“Yale maji ya uchungu yalimsaidia akaweza kujifungua mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo 1.7 na baada ya kujifungua alipoteza fahamu na saa 8:05 mchana akafariki dunia,”alisema.
Kwa mujibu wa Mrima, mtoto aliendelea kuishi huku akipewa maziwa lakini alikuwa akiyatapika, hadi ilipofika saa 5:00 usiku alifariki dunia
“Huwa tunasikia mtu anakufa baada ya kufunga ndoa lakini hili la wifi yetu kuwa siku ambayo ndiyo walipanga kufunga ndoa na kaka yetu limetushtua sana,”alisema dada huyo wa aliyetarajiwa kufuga ndoa na marehemu.
Baba mzazi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja tu, Mmasi aliwaomba waombolezaji kumuomba Mungu na kujiandaa kwani hawajui siku wala saa watakayotwaliwa.
Akizungumza katika mahubiri ya ibada hiyo, Padre Mavengero, alikemea chuki za kidini zinazoanza kupenyezwa nchini.
“Watu waishi vizuri kwa amani na wapendane waache kuchochea mfarakano wa kidini… Waislamu na Wakristo ni marafiki na ndiyo maana tumeshirikiana tangu Handeni hadi Rombo,”alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya harusi,Abdi Kipacha ambayo baadaye kamati yake
ilijigeuza kuwa ya msiba, alikabidhi kwa mfiwa Sh500,000 zilizokuwa zimetengwa kwa zawadi kwa ajili ya maharusi ambazo jana zilikabidhiwa kama rambirambi.Msiba huo umekuwa gumzo nchini hasa baada ya gazeti hili kuripoti tukio hilo lililotokea Handeni mkoani Tanga ambalo si la kawaida
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment