Thursday 25 July 2013

JESHI la Polisi la Kinondoni linatuhumiwa kumuua Selemani Mwinyi Msanga.

JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni linatuhumiwa kumuua Selemani Mwinyi Msanga, mkazi wa Kurasini, jijini Dar es Salaam akiwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Msanga anadaiwa kuuawa kati ya Julai 18-20 baada ya kukamatwa na askari wa jeshi hilo na kisha mwili wake kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Mwananyamala jana, ndugu wa Msanga, Joachim Mgende na Nasoro Msanga walisema Julai 18 walipata taarifa ya ndugu yao alikamatwa na kuambiwa wamfuatiliae katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Alisema siku ya kukamatwa kwa Msanga askari waliovaa kiraia walifika nyumbani kwa marehemu Kurasini na kufanya upekuzi huku wakiwa wanampiga na fimbo ya ufagio wakiochukua uani mwa nyumba hiyo.
Aliongeza wakati wa tukio hilo mtoto wa kufikia wa Msanga alishuhudia hali hiyo na kumpigia simu mama yake aliyekuwa eneo la Kigogo katika msiba na kumueleza kuwa baba yake amepigwa na kuchukuliwa katika gari na watu waliojitambulisha kuwa ni askari wanaotoka Oysterbay.

“Baada ya taarifa hizo wanandugu tulifuatilia huko Oysterbay tukaambiwa yupo Sitakishari nako tukaenda wakatuambia hajafikishwa, ilikuwa ni kuzungushwa tu mpaka tulipokuja kupata taarifa kuwa yupo chumba cha maiti Mwananyamala.
Alisema Julai 21 ikiwa ni siku ya nne kufuatilia hatima ya ndugu yao, dada wa marehemu alifika katika Kituo cha Oysterbay na kuonana na baadhi ya askari akiwamo mkuu wa kituo hicho, ambapo walimueleza kuwa hawana taarifa ya mtu huyo na kuwataka warejee kesho yake (Jumatatu) kwa taarifa zaidi.
Aliongeza kuwa baada ya taarifa hizo ndugu hao wakiwa wanajiandaa kuondoka kituoni hapo walifuatwa na mmoja wa askari wa kike na kuwaeleza kuwa ndugu yao amefariki dunia na kwamba mwili umehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala.
“Tulikaa kikao na kwenda Mwananyamala pale tukaomba kuuona mwili wa ndugu yetu huku tukisema polisi wametuambia umehifadhiwa pale. Kwa kweli hatukuweza kuutambua kwa urahisi, kwani ulikuwa umevimba na kupoteza uhalisia wake, kilichotusaidia ni kwamba baba mdogo alikuwa na alama usoni (sunzua) ndiyo tukamtambua,” alisema Nasoro.
Nasoro aliongeza kuwa kinachowasikitisha ni kuona Jeshi la Polisi linalotegemewa kuwa chanzo cha watu kufuata sheria likiwa mstari wa mbele kuvunja sheria.
Alisema hata kama ndugu yao alikuwa na tuhuma ambayo hawaifahamu, ingekuwa vema kama angefikishwa katika vyombo vinavyotafsiri sheria ili vimhukumu badala ya kukatisha uhai wake kwa njia ya kipigo.
Tanzania Daima ilifanikiwa kuona taarifa zilizotumika kwa ajili ya kuuhifadhi mwili wa Msanga katika chumba cha maiti ambazo zilikuwa zinaonyesha marehemu akiwa hajulikani jina na kwamba mwili wake uliokotwa katika eneo la Msasani.
Aidha, ripoti ya daktari iliyotolewa kwa ndugu wa marehemu ilionyesha kuwa sababu za kifo hicho hazijulikani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa juu ya kumshikilia Msanga na hatimaye kupoteza maisha akiwa kituoni alisema hana taarifa hizo na kwamba atazifanyia kazi.
Alipoulizwa kama anajua juu ya mtu aliyeokotwa katika eneo la Msasani akiwa amefariki dunia, pia kamanda huyo alisema atafanyia kazi na kutoa taarifa sahihi.
“Mimi siyo kamanda mbabaishaji na sifanyi kazi kwa kuendeshwa na mwandishi, nimekupokeeni nitafanyia kazi hayo mliyoniuliza na nitatoa majibu kwa ajili ya faida ya taifa,” alisema Wambura.
Wakati huo huo, wahudumu wa chumba cha maiti katika Hospitali ya Mwananyamala jana waliwakatalia askari wa Jeshi la Polisi kuingiza maiti katika chumba cha maiti kwenye hospitali hiyo kwa madai kuwa wamechoka kupokea miili ya watu waliokufa kutoka katika Kituo cha Oysterbay.
Tukio hilo lilitokea wakati waandishi wa habari wakipata maelezo juu ya madai ya kuuawa kwa Msanga, ambapo katikati ya maelezo hayo polisi waliwasili na mwili wa mtu na kutaka kuuhifadhi kabla ya kukataliwa na kuamua kuondoka nao.
Mmoja wa askari aliyeusindikiza mwili huo alisikika akiwaambia wenzie waondoke kwa kuwa miili inayotoka Oystebay Polisi haiwezi kupokewa katika hospitali hiyo.
Katibu wa hospitali hiyo aliyekataa kutaja jina lake, alipoulizwa sababu ya kukataa miili inayotoka Kituo cha Polisi Oysterbay alisema suala hilo hana taarifa nalo na kuomba apewe muda wa dakika tano afuatilie.
Baada ya dakika tano katibu huyo alirudi na kuwaeleza waandishi kuwa taarifa rasmi zitatolewa leo huku akisisitiza kuwa taratibu za hospitali lazima zizingatiwe katika kuhifadhi miili inayotoka nje.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment