Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambayo idadi ya wananchi wake wanaotumia nishati ya umeme ni ndogo sana.
Takwimu zinazotolewa na serikali mara kwa mara zinaeleza kuwa ni asilimia 17 tu ya wananchi wote wamefikiwa na umeme.
Idadi hii kwa hakika ni ndogo sana. Umeme ni moja ya nyenzo ya kuwaletea wananchi mabadiliko. Mwenye umeme amewezeshwa kukabiliana na changamoto za maisha, na hakika atashinda umasikini wake.
Kumekuwa na mkanganyiko juu ya takwimu halisi za Watanzania wanaopata umeme. Mwaka 2010 serikali ikijibu swali bungeni ilisema kuwa asilimia 14 ya Watanzania wanatumia nishati ya umeme, kati yao asilimia 12 ni watumiaji wa mijini na asilimia mbili ni watumiaji wa vijijini, takwimu hizi zilionyesha kuwa kati ya mwaka 2007 na mwaka 2010 kulikuwa na ongezeko la asilimia nne tu la watumiaji wa umeme. Takwimu hizi zinaweza kufafanuliwa kuwa ni ongezeko la asilimia moja kwa mwaka.
Wakati ongezeko la wananchi wanaopatiwa umeme likiwa ni la kusuasua hivyo, Waziri wa Nishati na Madini akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake bungeni Juni mwaka huu kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, alisema kumekuwa na miradi mingi ya umeme nchini ya kuharakisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Alisema kuwa hadi kufikia Aprili 2013 uwezo wa mitambo ya kufua umeme (installed capacity) ulikuwa MW 1,438.24. Katika uzalishaji huo, gesi asilia ilichangia asilimia 35, maji asilimia 39 na mafuta asilimia 26.
Uzalishaji huu kwa mujibu wa waziri husika ni ongezeko la asilimia 4.5 ikilinganishwa na takwimu za hadi Juni mwaka 2012 ambazo ziliponyesha kuwa uwezo ulikuwa ni MW 1,375.75.
Hata hivyo, waziri huyo alisema kuwa hadi kufikia Disemba 31, 2012 kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Gridi ya Taifa kilikuwa MWh 5,759,756 ikilinganishwa na MWh 5,153,400 mwaka 2011 sawa na ongezeko la asilimia 11.8, wakati mahitaji ya juu kabisa ya umeme kwa mwaka 2012/13 yalifikia MW 851.35 Oktoba, 2012 ikilinganishwa na wastani wa MW 820.35 kwa mwaka 2011/12. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 3.8. Alisema sababu kuu ya ongezeko hili ni kutokana na kukamilika kwa miradi mingi ya umeme vijijini.
Kwa maneno mengine, takwimu hizi zote zinazungumzia asilimia 17 ya Watanzania tu wanaopata umeme. Kama ni kufanya kila Mtanzania kupata umeme bila ongezeko lolote la shughuli za kiuchumi kwa hali iliyopo sasa ni sawa na kusema taifa hili linahitaji umeme mwingi sana. Ni sawa na kusema kuwa kazi ya kutafuta na kuzalisha umeme wa uhakika kwa kila Mtanzania, kwa kila shughuli ya uzalishaji mali bado ni mbichi kabisa.
Wakati hali ikiwa ni hivyo, kauli kwamba ifikapo mwakani Tanzania itaanza kuuza umeme nje ya nchi kwa sababu eti itakuwa na ziada kubwa ya MW 500, inaacha maswali mengi sana kwa umma kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja tu kuanzia sasa taifa hili katika sekta ya nishati ya umeme litakuwa limepiga hatua sana kiasi cha kuwafikia wananchi wote?.
Inawezekana sana Waziri amejawa na matumaini makubwa kwa sababu ya kugundulika kwa hazina kubwa ya gesi asilia nchini. Na kwamba kila akitazama mikakati ya kuisafirisha kwa mabomba gesi hiyo kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi, anaamini kabisa kwamba uzalishaji wa umeme utakuwa ni mkubwa sana nchini.
Si vibaya kuwa na matumiani, lakini ni hatari pia kuwaza kuuza umeme nchini kwa matumaini hayo kwa kuwa kazi ya ndani ya nchi ya kuhakikisha kuwa kila mkoa unafikiwa na mtandao wa Gridi ya Taifa bado ni kubwa mno, bado baadhi ya mikoa kama ya Kigoma, Rukwa, Katavi na Ruvuma haijafikiwa na umeme wa gridi. Kazi ya kuiunganisha bado sana.
Lakini hata kule ambako umeme wa gridi upo, kazi ya kusambazia wahitaji wote wa umeme bado ni changamoto ambayo kwa uhakika Tanesco imeshindwa kuitekeleza.
Maombi ya wanoataka kuunganishiwa umeme ni mengi kuliko uwezo wa Tanesco lakini pia makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji wa nishati yenyewe.
Mbali na hilo, hata waliounganishiwa umeme bado hawana uhakika na nishati hiyo. ukatikaji wa umeme ni wa kiwango cha juu sana. Kwa siku umeme unakatika saa nyingi tu. Kumekuwa na madai kuwa Tanesco wanaendesha mgawo ‘bubu’ yaani kimyakimya bila kutangaza kutokana na ukatikaji wa mara kwa mara wa nishati hiyo.
Kwa sasa hivi bado kazi ya kusafirisha hata hiyo gesi asilia kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam kwa maana ya kujenga bomba jipya nayo ipo katika hatua za awali sana.
Tunafikiri na kwa kweli tunaamini kwamba tupo sahihi kwamba badala ya serikali kuanza kuwaza habari ya kuuza umeme nje, ifikirie jinsi ya kuwafikishia wananchi wake wote umeme wa uhakika kwanza.
Kinachoonekana katika kauli ya waziri ni sawa na baba anayetaka kuuza chakula cha familia wakati bado mahitaji yao hajatoshelezwa.
Mipango kama hiyo haifai na ni hatari kwa ustawi wa familia, ndivyo ilivyo hata kwa taifa kwa mkakati huu alioutangaza waziri wiki hii
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment