Mahakama ya Mkoa wa Lindi, imewahukumu majambazi sugu wanne, wakazi wa jijini Dar es Salaam kifungo cha jumla ya miaka 240 baada ya kupatikana na makosa ujambazi.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Dustan Ndunguru, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Waliohukumiwa adhabu hiyo Bakari Abdallah Masoud, Hamis Majane Rashid, Mohamed Bakari Abdallah na Mohamed Said Kamkunde.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, washitakiwa walipewa nafasi ya kujitetea ambapo watatu kati yao waliiomba mahakama iwaonee huruma kwa madai kwamba ni kosa lao la kwanza na pia wana wazazi wanaowategemea.
Mshtakiwa Bakari Masoud, hakujitetea na badala yake alisema anaiachia mahakama itoe uamuzi utakaoona kwa upande wake unamfaa.
Baada ya utetezi huo, Mwanasheria wa Serikali, Juma Maige, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili liwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hiyo.
Hakimu Ndunguru aliwahukumu washtakiwa kwa kosa la kwanza la unyang’anyi wa kutumia silaha kila mmoja kifungo cha miaka 30 na kosa la pili la uporaji miaka 30 na hivyo kufanya jumla ya miaka 240 kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa vile adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, Hakimu alisema kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwanasheria wa Serikali, Juma Maige, kuwa Novemba 24, mwaka 2011, katika kijiji cha Mchichili, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, washtakiwa wote kwa pamoja wakiwa na bunduki na mapanga, walivamia dukani kwa Abdallah Said Kibuti, na kupora mali na fedha.
Pia washtakiwa walidaiwa kuingia chumba alichokuwa amelala dada wa Kibuti aitwaye Zawia, na kupora Sh. 100,000 na simu ya mkononi aina ya Nokia yenye thamani ya Sh. 50,000.
Mali nyingine walizopora washtakiwa hao ni fedha taslim Sh. 587,000, jozi 53 za vitenge aina ya waksi na java, jozi 42 za nguo mbalimbali zikiwamo za akina mama, suti za watoto jozi tisa na simu nne za mkononi aina ya Nokia, Jmax, Sumsung na Huwawei zote zikiwa na thamani ya Sh.1,105,000.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment