Yupo kijana mmoja aliyemuoa ampendaye wakaishi kwa miaka kadhaa huku wakiomba Mwenyezi Mungu awajalia mwana. Hata hivyo hilo halikufanikiwa ndipo mzozo ukazuka kila mmoja akimlaumu mwenzake kuwa ndiye tatizo.
Kwa kuwa walikuwa wamefunga ndoa, mzozo huo ulifikishwa hadi mahakamani ili waweze kuachana. Lakini wawili hawa walikuwa tayari wana mali ambazo ni nyumba na magari. Kila mmoja akadai agawiwe nusu kwa nusu mali zile walizochuma pamoja.
Lakini mashuhuda wanasema kuwa mwanaume huyo alikuwa ameendekeza sana ushirikina hivyo akaenda kwa waganga kumloga mkewe ili asahau mali zote. Hivyo ndivyo ilivyotokea, kwani mbali na mahakama kuamua kuhusu mgawanyo wa mali, lakini bibie tangu waachane na bwana huyo hakurudi nyuma kudai tena chochote.
Inasemekana bibie alienda kuolewa kwingine na maisha yake yanamwendea vyema.
Kwa upande wa mwanaume ndipo utamu wa habari hii ulipo kwani aliamua kuoa mwanamke mwingine haraka. Lakini mke huyu siyo wa rika lake bali mtu mzima ambaye anakaribia kuwa mama yake wa kumzaa. Si unajua tena tabia za mashuga mami(mama watu wazima) na mashuga dadi(baba watu wazima) kuoa dogodogo?
Wadadisi wa mambo wanasema kuwa mama huyu kabla ya kuolewa na bwana mdogo huyu, alikuwa ameolewa na kuzaa watoto wakubwa, miongoni wakilingana kiumri na kijana huyu ambaye sasa ndiyo mumewe.(Hii ilikuwa ni siri hakuijua bwana huyu).
Mama huyu mtu mzima baada ya kuolewa na kijana huyu, wakaishi kwa muda na ndipo akamwambia mumewe kuwa ni mjamzito.(Mama huyu alikuwa pandikizi, mnene ambaye ukiambiwa ni mjamzito mwenyewe utakubali tu). Kumbe ilikuwa ni uongo hakuwa na mimba wala nini. Ilikuwa ni fumbo mfumbie mjinga mwerevu alifumbue. Au siyo msomaji wangu.
Miezi ilivyosonga mbele akamwambia mume huyu kwamba anataka kwenda kwao mkoani akajifungulie huko ili apate huduma nzuri kwani pale walikuwa wakiishi wao wawili tu. Jamaa akaingia kingi akakubali na kumruhusu.
Kumbe alikuwa anakwenda kwao ambako yupo binti yake aliyekuwa mjamzito na tayari walishapanga na mama yake kuwa akijifungua tu atamchukua huyo mtoto ili aje amsingizie mumewe kuwa ndiye mtoto aliyezaliwa. Hilo likafanyika kwa usahihi kabisa.
Mama huyu mtu mzima baada ya muda akarejea hapa Dar kwa mumewe akiwa na mtoto huyo mchanga ambaye kiukweli ni mjukuu wake, (mwana wa bintiye) na siyo wake wa kumzaa.
Kurudi mumewe akafurahi kuona mama kajifungua mtoto, akampenda sana.(Bado hajajua hilo ni changa la macho) .
Mtoto huyu akakua hadi kuanza chekechea. Baba akimfurahia sana. Mpaka hapo huyu baba hajajua kuwa yule mtoto siyo wake. Ilifikia hatua wawili hawa wakabariki ndoa kanisani.
Na mtoto huyu kiukweli mama yake mzazi ambaye ni binti wa shugamami huyu, alimzaa na bwana ambaye waliachana na kurudi hapo kwa mama yake anakougulia. Ama kweli Maisha Ndivyo yalivyo.
Ikafikia wakati mama huyu mtu mzima(shugamami) akaugua. Hivi sasa yu hoi bin taaban hata kuongea haongei. Mume akachanganyikiwa kazi hana na huku anauguza.
Akaamua kuuza sehemu ya eneo analoishi ili kupata hela za kujikimu. Ile ameita mnunuzi, yule binti akamjia juu kwamba hana mamlaka ya kuuza. Akapiga ukunga(kelele), jambo ambalo lilivuta watu kujua kulikoni huku wakidhani pengine mama yule amefariki.
Kisha baba huyu akamtaka binti kuondoka nyumbani kwake kwa sababu yeye siyo baba yake na kwamba mwenye uhusiano naye ni mama yake ambaye wamefunga naye ndoa kihalali.
Baada ya binti huyo kuambiwa hivyo, alikuja juu na kumwambia baba yake huyo wa kambo kuwa hawezi kuuza kiwanja hicho wakati mama yake yuko ndani akiugua na yeye hawezi kuondoka hapo nyumbani kwa sababu ni kwa mama yake mzazi.
Yule baba akasisitiza ni lazima aondoke kwa sababu nyumba hiyo ni ya mtoto wake aliyezaa na mama yake huyo. Kauli hiyo ilizua mzozo na ndipo binti huyo alimtamkia bayana baba yake huyo wa kambo kuwa mtoto yule ni wa kwake na asidanganywe asilani kwamba ni wake aliyezaa na mamake.
Huyu baba hakukubali hilo kwa kuwa alimtunza mtoto huyo tangu mchanga na sasa yuko chekechea. Ingawa majirani walimgombeza binti yule kwa vurugu lakini tayari siri ilishawekwa hadharani.
Naam, inasemekana kwa matukio hayo yote, bwana kachanganyikiwa na binti hadi sana bado anavinjari pale anapougulia mamake huku akipigana kisogo na baba yake huyo wa kufikia. Na zaidi ni kwamba hivi sasa baba huyo anasaka mtu ili auze nyumba wanayoishi abadili mwelekeo wa maisha. Maisha ndivyo Yalivyo.
No comments:
Post a Comment