MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi dhidi ya jeshi hilo, vyombo vya dola na serikali kwa ujumla.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na Msemaji wake, Mrakibu Mwandamizi, Advera Senso, imesema kuwa Mbowe amekuwa akitoa kauli ambazo zimekuwa na mlengo wa uchochezi na kuijengea jamii taswira hasi juu ya vyombo vya ulinzi na usalama na kuwafanya wananchi kuwa na hofu.
Mbowe akiandamana na mawakili, Nyaronyo Kicheere na Peter Kibatara, alijisalimisha mwenyewe makao makuu ya polisi majira ya saa 8:30 mchana, mara tu baada ya kuwasili jijini kutoka safarini.
Hatua hiyo imetokana na kitendo cha polisi juzi usiku wa manane kuvamia nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na walipomkosa waliacha namba ya simu ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ili ajulishwe kwamba anahitajika.
Aidha, jana askari wengine kutoka Polisi na wengine wanaoaminika kuwa ni wa Idara ya Usalama wa Taifa walikwenda katika hoteli moja mjini Moshi walikoamini kwamba kiongozi huyo amejificha kwa nia ya kumkamata lakini hawakuambulia kitu.
Hata hivyo, wakati Mbowe akishikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma hizo, wenzao wa Mkoa wa Dar es Salaam wamedai polisi hawawezi kusumbuka kumkamata kiongozi huyo kwa mambo ya kisiasa.
Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ally Mlege, aliwaambia jana jijini Dar es Salaam waandishi wa habari kuwa polisi hawawezi kujiingiza katika malumbano ya kisiasa baina ya vyama hivyo viwili.
“Hatuna kauli yoyote kuhusu mivutano ya kuanzisha na kuendesha vikosi vya ulinzi na usalama inayoendelea ya kisiasa kati ya CCM na CHADEMA, jamani hayo ni mambo ya kisiasa,” alijibu Mlege.
Mbowe amehojiwa kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA kutaka kuanzisha kikosi cha vijana cha ulinzi cha Red Brigade na kauli ya kulituhumu jeshi hilo kumjua aliyehusika na bomu lililorushwa kwenye mkutano wa CHADEMA jijini Arusha na kuua watu wanne.
Mwenyekiti huyo pia anahojiwa kwa madai ya kulituhumu Jeshi la Polisi kuisaidia CCM katika uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha, pia madai ya kutoa kauli kwamba kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya kuhusiana na mauaji hayo, kunaonesha dalili za serikali kujua nani alihusika na tukio hilo.
Tuhuma nyingine ni madai ya kuhamasisha chuki kati ya jeshi na wananchi, pia kuchochea wakazi wa Mtwara katika sakata la gesi.
Mbowe ambaye alihojiwa takriban kwa saa tano, aliachiwa kwa dhamana na anatakiwa kuripoti tena Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Julai 23, saa 8 mchana.
Kauli ya CHADEMA
Kufuatia tukio hilo, CHADEMA wamesema kitendo cha kumkamata kiongozi huyo kimedhihirisha wazi kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuongoza nchi kwa mujibu wa sheria.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema hatua ya serikali ya kuwafungulia wapinzani tuhuma za uchochezi kwa kusema ukweli haina tofauti na vitendo vya serikali ya kikoloni iliyomkamata na kumfungulia mashitaka Mwalimu Julius Nyerere tuhuma kama hizo.
“CHADEMA kama ilivyokuwa TANU, tunashinda. Jeshi la Polisi ambalo askari na maofisa wake ni watuhumiwa wa mauaji si tu ya bomu na risasi Arusha, bali hata ya Mwangosi na mauaji mengine, isitumie madai ya uchochezi kuidhibiti CHADEMA na viongozi wake.
“Polisi kumhoji Mbowe siku chache baada ya kauli za Kikwete alizotoa kwenye mkutano wa TCD ni dalili kwamba wamesukumwa na mamlaka za juu yao. Jeshi la Polisi limshauri Kikwete kama anaona CHADEMA inasema uongo na uchochezi, basi aunde tume ya majaji ili ukweli ujulikane,” alisema Mnyika.
CHADEMA imesema chama hicho kimekuwa kikisimamia ukweli kuhusu mauaji yenye mwelekeo wa kisiasa tangu mwaka 2011, Arusha, 2012 Morogoro na Iringa na 2013 mkoani Arusha.
“Vyombo vya dola vikiwa ni sehemu ya watuhumiwa, ukweli huo unaitwa uchochezi na kutukamata badala ya watuhumiwa wa mauaji.
“Alichokisema Mbowe ni maamuzi ya Kamati Kuu na kama wanaona ni uchochezi basi wakamate wajumbe wote wa Kamati Kuu na wakishitaki chama,” alisema Mnyika ambaye katika kumsindikiza Mbowe aliandamana na Benson Kigaira na John Mrema.
Tendwa ashambuliwa
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemshambulia vikali Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kwa kile walichokiita ‘undumila kuwili’ kutokana na suala zima la ulinzi wa vyama.
Taarifa iliyotolewa na John Mnyika alisema Tendwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho Agosti 13, 2006, akiwa kama mgeni mashuhuri alibariki na kukubaliana na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na chama hicho.
Alisema moja ya mabadiliko yaliyofanywa na kuungwa mkono kwa pongezi na Tendwa ni uamuzi wa chama kuwa na chombo cha kulinda viongozi na mali za chama kitakachoitwa Brigedi Nyekundu.
“Tendwa katika hotuba yake alipongeza mabadiliko hayo ya katiba na ikasajiliwa katika ofisi yake mwaka 2006, baada ya kukubali kwamba imekidhi mahitaji yote muhimu.
“Leo anapogeuka na kuwaacha polisi kuadhibu viongozi wetu kwa kile alichokiunga mkono wakati ule ni jambo la kusikitisha sana na lenye lengo la kufuata mkumbo wa kauli ya Kikwete na polisi badala ya kuzingatia katiba na sheria za nchi.
Mnyika alisema badala ya Tendwa kuitishia CHADEMA ambayo haijavunja sheria, ingekuwa bora akakifuta Chama Cha Mapinduzi.
“Hiki kimevunja sheria katika chaguzi ndogo za Kiteto, 2007, Tarime 2008, Busanda na Biharamulo 2009, Uchaguzi Mkuu 2010, Igunga 2011, Arumeru 2012 na za marudio kwenye kata 21, mwaka 2013 kote nchini.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukieleza kuhusu makambi ya Green Guard yanayofanya mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kufanya mashambulizi na matukio kwa Wanachadema na wanahabari.
“Mathalani mbali ya kushambuliwa CHADEMA, Green Guard ya CCM imewahi kuwashambulia waandishi wa habari, Frederick Katulanda wa Mwananchi mwaka 2010 katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, Musa Mkama wa Dira ya Mtanzania huko Igunga katika uchaguzi mdogo 2011, Munir Zacharia wa Channel Ten huko Zanzibar katika uchaguzi mdogo wa Bububu na ushahidi wa hayo upo,” ilimaliza taarifa hiyo
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment