Thursday 18 July 2013

Mtwara kwawaka moto tena

MZIMU wa vurugu na hasira za wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara umeibuka tena jana baada ya wananchi wenye hasira kuwavamia na kuwashikilia viongozi wa vyama vya ushirika Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Wakulima hao wakiwa na hasira huku wakiapa kukabiliana na nguvu yoyote ya serikali, wamewakamata na kuwafungia viongozi wawili wa Chama cha Ushirika wa Nanyamba katika ghala la korosho kwa zaidi ya saa nane, kabla ya kuokolewa na polisi.
Habari za kuaminika na zilizothibitishwa na uongozi wa polisi wa wilaya, zimesema kuwa wakulima hao wenye hasira walimzuia mwenyekiti wa ushirika huo aliyefahamika kwa jina moja la Nantolela na katibu wake, Lipaike ikiwa ni njia ya kuishinikiza serikali iwalipe malipo yao ya pili ya korosho.
Wakiongea kwa hasira na bila utaratibu, wakulima hao wamesema wamechoshwa na ufisadi wa viongozi wa vyama vya ushirika wanaojinufaisha na pesa za wakulima ambao wanafumbiwa macho na serikali kwa muda mrefu.

“Hatuwaachi hadi kieleweke, tulipwe pesa zetu, utani wa aina hii unaofanywa na serikali kushindwa kufuatilia viongozi hawa wanaojinufaisha na jasho letu umetosha, tunataka haki yetu, tunasomesha, tuna mahitaji yetu.
“Hii ni kejeli kubwa, tuliwakopesha korosho tukalipwa malipo ya awali shilingi 600, wengine sasa wanadai 600 zingine, wengine wanadai 400, wengine wanadai 200 kutegemeana na walivyolipwa, korosho za wakulima wamekopa na wameshauza maghala hayana korosho, na pesa hazionekani,” alisema mmoja wa wakulima hao.
Fujo hizo zilizotokana na hatua ya serikali wilayani humo kutaka kuwalipa wakulima hao sh 15, tu za malipo ya pili kwa kilo ya korosho, badala ya kulipwa kati ya sh 200 na 600 kama ilivyokubaliwa katika kikao cha Juni 27, mwaka huu.
“Kikao kilichofanyika tarehe 27 Juni tulikubaliana kulipwa, tumeambiwa viongozi wetu walienda benki wamekopeshwa pesa na sasa wametuita kutaka kutulipa shilingi 15, tu kwa kilo badala ya 600 au 300 au 200 kadiri tunavyodai,” alisema mkulima mmoja huku akishangiliwa na wenzake.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile alisema: “Niko njiani, naelekea Mtwara sina majibu kwa sasa ingawa tayari tulitoa amri kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuwalipa wakulima pesa zilizosalia, sasa hilo la Nanyamba sijalisikia vema, nadhani labda bado kuna viongozi wanasumbua wakulima, nitajitahidi nikifika Mtwara nikupe majibu kuhusu suala hilo hapo kesho.”
Mkuu wa Kituo cha Polisi Nanyamba alikiri kufungiwa kwa viongozi hao tangu saa 3 asubuhi hadi saa mbili usiku alipofika huko kuwaokoa na kuamrisha kuwa wakae na diwani ili kuhakikisha wakulima hao wanalipwa.
“Ni kweli walifungiwa na wakulima, nilifika pale kuwaokoa wasidhuriwe ila sasa kuhusu malipo sikufuatilia maana hiyo sio kazi yangu,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hana taarifa kwa kuwa yupo mkoani Mbeya kwa matatizo ya kifamilia.
Hali hiyo inajitokeza ikiwa ni miezi michache tu tangu kundi la wakulima wa Korosho wilayani Liwale mkoani Lindi, walipojaribu kuzuia gari lililokuwa na fedha za malipo ya korosho wakipinga kiasi kidogo cha malipo yao ya pili na kuanza kufanya vurugu na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Kutokana na vurugu hizo zilizotokea Aprili 23 mwaka huu majira ya saa tisa alasiri, nyumba zaidi ya 10 zilichomwa moto zikiwemo za wabunge na viongozi mbalimbali na mali kadhaa kuharibiwa.

No comments:

Post a Comment