Monday, 15 July 2013

MWEEEEEH!!!! Unamwibia mwenzio mume, anafariki halafu unatafuta ndugu zake kwa yule uliyemwibia!

Kisa cha jamaa mmoja aliyekufa lakini akazikwa bila kujulikana na ndugu zake ni akina nani. Hebu leo kaa mkao wa kula nikumegee kituko hicho na kama utakuwa na maoni au ushauri ujiachie bila wasiwasi ili sote tuelimishane. Au siyo? We haya wee!
Mama mmoja kafiwa na bwana aliyekuwa akiishi naye bila kujua ndugu za mwanaume huyo wanaishi wapi. Siku mbili kabla ya kifo, wakati anaumwa, huyu mama alizinduka na kumuuliza bwana amuelekeze wapi waliko ndugu zake ili akawape taarifa waje kumuona.
Bwana akamjibu; unadhani maisha haya magumu nani ataacha kazi zake aje kuniona? Wewe niuguze nikifa unizike. Baada ya kufariki mama huyo akataharuki na kuyakumbuka yale maneno “nikifa nizike”.
Baada ya kufariki yule mama akayafikiria yale maneno kwa kuwa hakujua kama itatokea kuwa kweli! Sasa yakaibuka makubwa yafuatayo;
Kumbe huyu mama alimpokonya mwenzie huyo bwana kwani pale msibani watu walishauri afuatwe yule mama aliyeporwa bwana ambapo alipoendewa akaambiwa kuwa yule bwana uliyekuwa ukiishi naye amefariki. Kisha wakamuuliza kama anawajua ndugu zake. Naye akawajibu tulijuana kimjini mjini.
Baada ya kupata maelezo hayo waombolezaji wakawa hawana cha kufanya hivyo marehemu akazikwa na waumini” Hivi ndivyo anavyomaliza ujumbe wake msomaji wetu huyu.
Mpenzi msomaji wangu, mambo ndiyo mambo. Umekielewa vyema kisa hiki? Hapa yapo mambo mawili yaliyojitokeza; Kwanza mwanaume aliyefariki lakini ndugu zake hawajulikani waliko. Pili, bwana huyu aliyefariki aliporwa kutoka kwa mwanamke wake wa awali.
Angalia pointi hiyo ya kwanza, inashangaza kwanini jamaa tangu anaishi na mwanamke huyu aliyemfia, hakuwahi hata siku moja kumtambulisha kwa ndugu zake. Hapa lipo tatizo.
Na ndiyo maana hata pale alipomsihi amfahamishe kwa ndugu zake ili awataarifu ugonjwa hakutaka na badala yake akamwambia wewe niuguze nikifa unizike, jambo ambalo limetokea.
Halafu pointi nyingine ni ile kwamba kumbe mwanaume huyu alikuwa na mwanamke mwingine kabla ya huyu aliyemfia. Na mwanamke huyu mwingine alikuwa akifahamika na baadhi ya watu na ndiyo maana baada ya kufariki ulitolewa ushauri pale msibani kwamba atafutwe yule mwanamke wa awali aulizwe pengine atakuwa anawafahamu baadhi ya ndugu za mwanaume huyo marehemu.
Lakini napo katika hali ya kushangaza, naye akajibu kwa jeuri kwamba hawajui na kwamba yeye na huyo bwana walikutana kimjini mjini.
Mpenzi msomaji, hata vijana huko mtaani wana maneno yayo ambayo huyatoa kwa utani lakini wakati mwingine huwa kweli, kwamba “tulikutana kimjiji mjini na tutaachana kimjini mjini”. Upo hapo? Maisha Ndivyo Yalivyo. Kaa chonjo na jirekebishe kwani leo kwangu, kesho kwako!
Hapa yapo mengi ya kujifunza. Watu wabadilike na wawe wawazi wanapokuwa katika mahusiano. Hakuna sababu ya mtu kuishi na mwenzie bila kujua ndugu zake. Huu ni utamaduni wetu tangia enzi za mababu kwamba watu kufahamiana hata kama siyo ndugu zako ni jambo la faraja na neema pia.
Kwanini mtu afiche ndugu zake? Hata kama ulikosana nao angalau waonyeshe basi ili ikiwezekana kuombeana msamaha.
Ni muhimu kumuomba mwenzako msamaha, kama atakusamehe ni vyema na kama hakukusamehe hiyo ni shauri yake maadamu umetimiza wajibu wako wa kumuomba msamaha.
Kama kwa Mungu kuna msamaha, mwanadamu yeye ni nani asiyesamehe? Kama Mungu hukusamehe wewe, kwanini mwenzio akikukosea usimsamehe? Tafakari na uchukue hatua.

Mpenzi msomaji, nimechangia vya kutosha. Ngoja nikuachie nawe utoe maoni yako kuhusu kisa hicho kisha tuelimishane pamoja.
Chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment