Thursday 18 July 2013

Vijana wanahitaji uhuru wa ngono kuliko wa kiuchumi?

VIJANA wengi hawako huru kwa sababu hawajitegemei kiuchumi na badala yake wanategemea shilingi ya mtu.
Vijana wengi ni tegemezi, wanawategemea wazazi, ndugu na walezi ili wawasaidie kupata mahitaji yao ya msingi kama chakula, mavazi na malazi.
Bado hawajawa huru kutokana na hali zao za kiuchumi, wanashindwa kujimudu wenyewe, wengine bado wamo masomoni.
Katika hatua ya ujana ndipo vijana hujenga taswira ya maisha yake na msingi wa maisha ya baadaye.
Mara nyingi vijana ambao wako katika hali ya utegemezi huelekeza fikra zao kuwaza ngono, jambo linalowagharimu huku wakijikuta wanahitaji uhuru wa ngono kuliko wa kiuchumi.
Ukijaribu kukaa nao na kuwasikiliza mazungumzo yao, utagundua ninachomaanisha, hata malalamiko yao kwa wazazi ni kunyimwa uhuru wa kuwa na mahusiano ya ngono na si kunyimwa uhuru wa kufanya shughuli za kiuchumi za kuwaingizia kipato.
Ni hatari sana kama vijana watahitaji na kukimbilia uhuru wa ngono zaidi kuliko uhuru wa kiuchumi, taifa litaendelea kuwa na idadi kubwa ya vijana tegemezi kutokana na fikra, mitazamo waliyonayo na mienendo yao ya kuweka kipaumbele masuala ya ngono.
Vijana hawa hutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, matokeo yake vijana wanazidi kuwa tegemezi na kuwa mzigo unaoelemea familia, jamii na taifa, pia kuwa na mchango mdogo katika kuchangia uchumi wa taifa kiasi cha kudharauliwa na kutothaminiwa.
“Mtu yeyote asiudharau ujana wako,” maandiko matakatifu yanaeleza hivyo lakini jiulize kwanini vijana wengi wa siku hizi wanadharaulika na kupuuzwa?
Tatizo ni wao wenyewe kabla ya kuanza kulaumu serikali, wazazi na jamii? Tukae chini kujitafakari na kujitathmini kuwa mitazamo, fikra, mienendo yetu na mielekeo iko sawa.
Haiwezekani vijana wanatumia muda mwingi kuwaza ngono, huku wengine wakimaliza muda wao kwenye mitandao ya kijamii kutafuta wapenzi na taarifa zinazohusu ngono kuliko kutafuta maarifa yatakayowatoa katika uchumi tegemezi na kuwafanikisha kimaisha, wachache sana utawakuta wanafanya hivyo.

Yapo mambo ya msingi katika maisha si tu kuipa ngono kipaumbele. Sikatai kuwa ina sehemu yake katika maisha lakini ni kwa wakati wake, umri wake na mtu sahihi wa kushirikiana naye katika hilo, hususan kwenye mpango maalumu kwa maana ya ndoa.
Ni vema vijana wakatambua kuwa Mungu alivyowaumba alikuwa na makusudi yake na iko kazi wanayotakiwa kuifanya na kuikamilisha kwa kuangalia vipaji vyao.
Mungu hajakuumba uwe mtumwa wa ngono. Tatizo la vijana kupenda uhuru wa ngono kuliko wa kiuchumi limekuwa likiwasababishia kuwa katika hali mbaya kiuchumi na kuendelea kuwa tegemezi, kwa sababu mabadiliko yanaanzia kwenye fikra kama mawazo yao.
Fikra zao zimejaa ngono, ni vigumu mtu huyu kujikwamua kiuchumi kwa sababu hatakuwa na kiu ya kutafuta mafanikio ya kiuchumi, sanasana anatafuta namna ya kuzitosheleza tamaa za mwili wake.
Uhuru wa vijana usiwe sababu ya kufuata tamaa za mwili, mbaya zaidi kijana anapotoka nyumbani na kwenda kuanza maisha yake, wengi wanasukumwa kwenda kujipatia uhuru wa ngono na si kuwa huru kwa ajili ya kufanya shughuli za kujikwamua kiuchumi na kujitegemea ili aweze kutegemewa baadaye na wazazi, ndugu, rafiki na jamii.
Huu ni mwendelezo wa mtazamo ambao alishaujenga tangu alipokuwa tegemezi, hivyo lengo lake kuu linakuwa ni kuwa na uhuru wa namna hiyo.
Nidhamu ya fedha kwa vijana inakuwa ndogo sana ni waponda raha, vijana wa zamani wanasema: “Vunja mifupa kama meno bado iko.”
Umri unakwenda mbele, hakuna walichokifanya, maisha hayabadiliki, wako vile vile maisha yote kutokana na misingi mibovu waliyojiwekea kabla ya kuanza maisha.
Kwa misingi hii na mitazamo hasi wanayokuwa nayo vijana kabla ya kuanza maisha ni vigumu kufanikiwa kiuchumi kwa sababu uhuru aliotamani kuufikia na kuuendea ni wa ngono na si wa kiuchumi baadaye.
“Wanakosa chaguo na kuwa na wapenzi wengi kama nguo, wanawasweka kwenye kabati na kuwabadilisha kama nguo.” Haya ni baadhi ya maneno ya wimbo kutoka kwa msanii Fareed Kubanda kutoka Mwanza.
Maisha hayawezi kusogea mpaka uyasogeze, vijana wanapaswa kujua kwamba maisha yao hayawezi kusogea hadi wenyewe watakapochukua hatua na kuyasogeza, hakuna mtu atakayewasogezea maisha yao kwenye mafanikio isipokuwa wao wenyewe.
Sijui vijana wanasubiri nani awasogeze katika mafanikio?
Tuache kujihusisha katika mambo ambayo hayakupeleki kwenye mafanikio na kufanya maisha yako yasogee zaidi ya kupoteza muda.
Ujana ni tunu inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kutumika vizuri, wahenga walisema maisha fainali ni uzeeni, ukichezea ujana wako vibaya majuto yanakuja baadaye kama Waswahili wanavyosema kuwa majuto ni mjukuu.
Uhuru ni kufanya mambo sahihi na wakati nchi yetu inapata uhuru kaulimbiu ilikuwa ni: “Uhuru na kazi” chini ya uongozi wa hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye wakati huo alikuwa kijana.
Lakini kwa sasa hali ni tofauti kwa vijana, wakipata uhuru cha kwanza wanachofikiria ni ngono, kazi baadaye.
Kwa mantiki hii mafanikio ya kiuchumi yatabaki kuwa ndoto za mchana kweupe.
Pesa inaleta uhuru, japo pesa si kila kitu na pia pesa haimafanyi mtu kuwa na furaha wala huzuni inategemea na uhuru wa kifedha alionao jinsi atakavyoutumia, matokeo yake ndiyo yanaweza kuleta furaha ama huzuni.
Uhuru wa kiuchumi ni mzuri kuliko uhuru wa ngono, uhuru wa kiuchumi unamfanya mtu aweze kuheshimika na wazazi, ndugu, rafiki na jamii, mtu akiwa huru kiuchumi hawi tegemezi na anaweza kuwasaidia na watu wengine pia.
Mchango wake unahitajika hata kwa jamii inayomzunguka. Anakuwa anathaminiwa pia kwa kuzingatia umuhimu wake.
Kama vijana wataendekeza ‘fashion’ ya ngono na kuipa kipaumbele zaidi ni vigumu kwa wao kuheshimika na kuthaminiwa, watabaki kuwa tegemezi.
Ni vema vijana wakatamani uhuru wa kiuchumi kuliko uhuru wa ngono na kujikita huko ili kurudisha heshima yao katika familia zao, ndugu, rafiki, jamii na taifa kuliko uhuru wa ngono ambao mara nyingi unaleta fedheha na si furaha wala uhuru kama wengi wanavyodhani.
Uhuru wa ngono si uhuru halisi kwa vijana kama wanavyodhani, ukifanya uchunguzi wa kina utagundua kuwa katika mahusiano ya ngono hakuna uhuru kwani mara nyingi yametawaliwa na hofu na wasiwasi ndani yao.
Vijana wengi hususan wanafunzi wa sekondari na vyuo huwa wanahofia mimba, maradhi na wasiwasi wa kuachika kwa kuhisi kwamba aliyenaye ana mpenzi mwingine.
Kwa asilimia kubwa mahusiano hayo yanaishia kwenye maumivu (kubwagana), uchungu, chuki na kuwa watumwa wa ngono huku wengine wakipoteza dira ya maisha.
“Utanashati na furaha ni muonekano wa nje kwa wanaojihusisha na mahusiano ya ngono (wapenzi) lakini ndani yao kunaonesha walivyowafungwa wa ngono, utadhani wana furaha kwa nje huku ndani yao wamejaa hofu na wasiwasi,” kinaeleza kitabu cha 24 Fundamental Sex Question Bothering people today, kilichoandikwa na Adah Nyinomujuni.
Kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa lengo la kuletea maendeleo na kuwasaidia wengine, natamani kuona vijana wakishindana kiuchumi na si kuwa na wapenzi wengi.
Jamii haipendi kuona vijana wakishindana katika mitindo ya mavazi na nywele, mambo ambayo hayawasaidii kuandaa kesho nzuri (maisha mazuri ya baadaye).
Mwanaharakati Malcom X anasema?: “Maisha ya baadaye yanawahusu walioyandaa leo.”
Hivyo kama hujajiandaa leo ujue kesho si ya kwako, utabaki kung`aa macho wenzako wanapiga hatua, utabaki kulaumu na kujilaumu tu.
Kila kijana atafakari kuwa anayoyafanya leo yatampeleka katika kesho anayoitaka, maana kila mtu huvuna akipandacho na tofauti na hapo ni uendawazimu wa kufanya kitu kile kile kwa namna ile ile na kutegemea matokeo tofauti.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment