Thursday, 8 August 2013

Bilionea wa madini auawa kwa risasi KIA




MFANYABIASHARA maarufu wa madini aina ya tanzanite jijini Arusha, Erasto Msuya, ameuawa kikatili kwa kumiminiwa risasi takriban kumi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Tukio hilo lililogubikwa na utata wa hali ya juu kutokana na mazingira yake, lilitokea jana mchana eneo la Mijoholoni, wilayani Hai, wakati marehemu akiwa njiani kutokea Arusha.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, zilisema kuwa mfanyabiashara huyo bilionea alikutwa na mauti hayo akiwa na gari lake la kifahari aina ya Range Rover lenye namba za usajili T 800 CKF.
Hata hivyo, Kamanda Boaz hakuweza kutoa taarifa zaidi  juu ya mauaji hayo kutokana na kile alichodai alikuwa akielekea eneo la tukio na kuahidi kutoa taarifa mara baada ya kurejea kutoka eneo hilo la tukio.
Taarifa zaidi zilizolifika zilidai kuwa Msuya alipigwa risasi na watu wawili waliokuwa wamepanda pikipiki na kupita eneo alilokuwa amesimama nje ya gari lake akizungumza kwa simu.
Baadhi ya marafiki zake jijini Arusha waliokuwa naye muda mfupi kabla ya tukio hilo walidai kuwa alipigiwa simu akiitwa eneo hilo kwa ajili ya kumuuzia madini.
Katika hali inayoacha maswali kuhusu tukio hilo, wauaji hao hawakuchukua kitu chochote kuanzia gari, fedha sh milioni 100 zilizokuwa ndani, simu za mkononi pamoja na ipad.
Chanzo chetu cha habari kilidokeza kuwa tukio hilo huenda limepangwa ili kuzima vuguvugu la tuhuma za mauaji ya mchimbaji mmoja aliyeuawa hivi karibuni kwenye machimbo ya Mererani.
Kwa mujibu wa watoa habari walioomba kuhifadhiwa majina yao, sakata la kesi hiyo limekuwa na utata mkubwa kutokana na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kutaka kumkumbatia mtuhumiwa wa mauaji hayo, kwa kutomfikisha mahakamani.

Marehemu Msuya anatajwa kama mmoja wa wachimbaji waliokuwa mstari wa mbele kuwashinikiza polisi kuhakikisha kesi hiyo inafikishwa mahakamani ili haki itendeke kwa wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Tukio hilo limeanza kuibua hofu miongoni mwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara juu ya kurejea kwa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha uliokuwa umepoa kwa muda katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Tanzania Dama jana, wamedai kuwa tukio hilo bado limegubikwa na utata kutokana na mazingira yake, kwani gari la marehemu lilikutwa limeegeshwa pembeni mwa barabara kuu ya Arusha - Moshi kana kwamba kulikuwa na mazungumzo baina ya marehemu na wauaji
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment