Pages

Tuesday, 27 August 2013

Gurumo: Nimestaafu muziki sina hata baiskeli

Gwiji wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Gurumo (73) ametangaza rasmi kuacha kujishughulisha na muziki baada ya kuitumikia fani hiyo takribani miaka 53.

Gurumo alitangaza kustaafu muziki huo jijini Dar esSalaam jana wakati alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema ameamua kuachana na muziki huo kutokana na umri kumtupa mkono pamoja na maradhi ya mara kwa mara, lakini licha ya hivyo bado ataendelea kutoa ushauri wa muziki katika bendi yake ya Msondo Ngoma na kwa wanamuziki wengine nchini watakaohitaji ushauri kutoka kwake.

“Leo nimekuja kuwaaga rasmi wanamuziki na mashabiki wangu kwa ujumla, na nimeamua kustaafu kwa moyo mmoja, pia kustaafu kwangu hakuzuii kutoa ushauri katika bendi ya Msondo na kwa wanamuziki wala kufundisha wapiga ala kwani nina kipaji cha kumfundisha mpigaji wa chombo chochote kwa kutumia mdomo wangu,” alisema Gurumo.


Gwiji huyo alisema kuwa alianza kuimba muziki tangu akiwa na umri wa miaka 20 hivyo ni fani anayoijua vema na tangu hapo hajawahi kujishughulisha na kazi nyingine yoyote.

Aliongeza kuwa licha ya kuutumikia muziki kwa miaka mingi kwa moyo wake wote lakini anastaafu akiwa hana kitu chochote cha maana alichokipata kupia tasnia hiyo.

“Nilianza kuimba tangu mwaka 1960 kipindi hicho nikiwa kijana mdogo wa miaka 20 na tangu hapo sijawahi kujishughulisha na kazi nyingine yoyote lakini leo hii nastaafu mimi Gurumo sina hata baiskeli,” alisema gwiji huyo.

Akitofautisha muziki wa dansi wa zamani na wa sasa alisema wanamuziki wa zamani walikuwa wakiimba muziki wenye mahadhi ya kinyumbani tofauti na sasa ambapo wanaimba mahadhi ya nchi nyingine hasa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Nawaasa wanamuziki wa dansi nchini wapige muziki wa nyumbani hasa tuliokuwa tukiupiga katika bendi ya Msondo na wala si kuiga kutoka katika nchi nyingine, ingawa hivi sasa kuna aina mbalimbali za muziki ikiwamo Bongofleva ambao wanamuziki wengi wanakimbilia huko kwa kuona ndiyo unakwenda na wakati lakini huo ni wa kupita tu,” alisema Gurumo.

Gurumo alisema kuwa katika nyimbo alizowahi kuimba wimbo anaoupenda ni wimbo wa ‘Usimchezee Chatu’, ambao aliuimba kipande kidogo mbele ya waandishi wa habari wakati kwa wanamuziki wa Bongofleva alisema anampenda Naseeb Abdul ‘Diamond’ kwa wimbo wake 'Nenda Kamwambie'.

Kwa upande wake, Meneja wa Msondo, Said Kibiriti alisema kuna tamasha maalumu litakaloandaliwa kwa ajili kumuaga msanii huyo huku mratibu wa tamasha hilo atakuwa ni Juma Mbizo, mratibu mkongwe nchini wa matamasha mbalimbali na muanzilishi wa viota na kumbi nyingi za burudani jijini Dar es Salaam.

Pia alimtaja Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka, mdau wa burudani Said Mdoe, Richardson Sakalla, mkurugenzi wa bendi ya The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’, Waziri Ally kuwa ndiyo miongoni mwa wanakamati iliyoundwa ambayo Gurumo ameiafiki ili imsaidie kuandaa tamasha hilo.

Mratibu wa tamasha hilo, Mbizo alisema watatoa taarifa kupia vyombo vya habari kuhusu mahala na siku itakayofanyika tamasha hilo na watataja vitu walivyomuandalia kumfanyia mwanamziki huyo.

“Kamati hii imeundwa ili imsaidie katika kumuandalia tamasha maalum la kumuaga na yeye kuaga mashabiki wake, kwa yeyote anayeguswa na suala hili anaweza kumchangia siku hiyo ya kumuaga.

Siku hiyo ataimba kwa mara ya mwisho na kuanzia leo hatapanda tena katika jukwaa lolote kuimba,” alisema Mbizo.

Gurumo ambaye alizaliwa mwaka 1940, alianza muziki mwaka 1960 katika bendi ya Kilimanjaro Chacha. Mwaka 1962 alijiunga na Rufiji Band kabla ya kutua Kilwa Jazz mwaka 1963.
Mwaka 1964 akawa muasisi wa NUTA Jazz ambayo ndiyo kwasasa inaitwa Msondo Ngoma Music Band aliyodumu nayo hadi sasa.

Licha ya kudumu Msondo hadi sasa, mwaka 1978 alikwenda kuanzisha bendi ya DDC Mliman Park 'Sikinde', kisha Orchestra Safari Sound (OSS) na mwaka 1990 alirejea tena Msondo.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment