Friday 23 August 2013

Kamati ya Bunge yabaini ufisadi Wizara ya Magufuli

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema kuwa taarifa ya matumizi ya fedha katika Wizara ya Ujenzi, ina shaka kwani kuna  fedha ambazo ziliombwa kwa ajili ya miradi ambayo haipo. 

Hayo yalibainishwa jana katika kikao cha kamati hiyo pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Ujenzi.

Gaudence Kayombo, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho cha kamati  kilichofanyika jana katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, alisema baada ya kupitia taarifa ya wizara hiyo, waliona kuna  Sh. bil. 348 ambazo ziliombwa na wizara hiyo kwa mradi ambao hauonekani.


Alisema  katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo mwaka juzi, ilionyesha kwamba kiasi hicho cha fedha kiliombwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara na siyo kama ilivyoelezwa kwenye taarifa iliyopitiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na kamati hiyo.

Kayombo alisema kuwa, katika taarifa hiyo iliyoletwa mbele ya kamati hiyo ilieleza kuwa sehemu ya kiasi hicho cha fedha kilitumika kwa ajili ya kuwalipa makandarasi ambao wanawadai tofauti na maelezo yaliyopelekwa bungeni katika kipindi hicho.

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Herbert Mrango, alisema kuwa, katika kiasi hicho walichoomba, bunge lilipitisha  Sh. bil. 253  na kwamba kati ya hicho kilitumika kuwalipa makandarasi hao ambao wanaidai wizara hiyo kwa madai ya kwamba wanapolipwa, kazi ya ujenzi wa barabara inakwenda haraka.

Hata hivyo, wajumbe wa kamati hiyo waliihoji wizara hiyo kwanini wanatumia fedha za serikali kinyume na taratibu za maelezo ya kibajeti yanayopelekwa bungeni.

Aidha, kamati hiyo iliitaka wizara hiyo kuonyesha wazi kiasi kamili cha fedha wanachoomba kwa ajili ya kulipia madeni wanayodaiwa na makandarasi wa barabara kwenye bajeti ya serikali wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment