Monday, 26 August 2013

Mke amtaka mume aache kazi, alipokataa akatimka!

kuna visa vingine ukivisikia, unafananisha kabisa na mchezo wa kuigiza kumbe ni kweli. Hivi mtu mwenye akili timamu anaweza kumwambia mwenzake (mke na mume) acha kazi wakae tu wanatizamana?
Huwezi kuamini, wapo watu wa aina hii lakini binafsi nikiamini kuwa siyo utashi wao bali msukumo toka anga zingine zisizo na nia njema. Au niishie kusema tu kwamba pengine ni ufinyu wa fikra unaotokana na malezi/makuzi au tabia ya ujinga asiyetaka mabadiliko katika maisha yanayomzunguka.
 kituko ambacho kilimkuta yeye mwenyewe kwa mkewe kumlazimisha aache kazi na alipokaidi mke yule akaishia zake na sasa analima vibarua vya shamba kwa watu na mumewe mpya.
Si unajua ule msemo kwamba mtu anaruka mkojo anakwenda kukanyaga mavi, au mkataa jema pabaya panamwita? Hayo yamemkuta bibie huyo aliyemwacha mume mchakarikaji ili familia iishi maisha bora, akaishia kwenda kuolewa na mtu anayebangaiza kwa kulimishwa mashambani ili mkono uingie kinywani. 
 Mimi naitwa Joseph au Kibaden Limo ni mchaga wa Kibosho nimeamua kukuletea stori hii ili unipe ushauri.
Mimi nimemuoa mwanamke wa Kisambaa, nikaishi naye miaka miwili, nikazaa naye mtoto wa kiume. Nikaenda kwao Tanga kuwafahamu wazazi wake, nikamtolea nusu ya mahari kama ilivyo desturi.
Basi tukarudi salama nyumbani kuendelea na maisha kwa kuwa maisha ni kupambana kila kona. Nilimwachia duka mimi nikaamua kwenda kusaka kazi kwa bahati namshukuru Mungu nilifanikiwa kazi ya kupandisha watalii mlimani Kilimanjaro kama muongozaji(guide).

 ndipo machungu yalianza tena makali. Nilipofikisha miezi sita, mwenzangu akaanza kuleta taabu eti niache kazi. Kuhoji akasema eti sababu nina hawara. Nilishangaa sana. Nikamjibu nakupenda sana mama fulani hakuna nikikosacho kwako. Au wivu? Akadai amekwisha kusema ama nimpe nauli asepe zake.
 nikaamua kumtizama tu atafanya nini nikaenda kazini kama kawaida ambako hukaa siku saba ndipo narudi nyumbani. Akawa bubu, hakuna pole wala salamu, nikampa hai naye kimya.
Nikauliza mama fulani vipi? Mbona hivi? Nikamwita ndani nikamwambia ni nani anayekuharibu namna hiyo…jibu akasema nitengeneze kama nimeharibika. Nikaamua kumweleza mama yangu mzazi akatukalisha lakini haikusaidia kitu…majibu, anasisitiza niache kazi ya mlima la sivyo nikienda huku nyuma naye anaondoka.
Akabadilisha ratiba kabisa akaamua kulala kwenye kochi, nikamsihi kila ushauri na maneno matamu nikaambulia kashfa na matusi. Nilikasirika nikalia sana kwa kuwa mtoto wetu bado mdogo na sikumpiga hata kofi moja lakini nasikia harufu ya damu.
Nikatoka nje Mungu akasikia kilio changu nikaenda kufanya kazi moja nzito nikapata pesa nzuri. Kurudi nyumbani hayupo kipenzi nimpendaye Halima wangu kupiga simu hapokei. Kupiga kwao mama mkwe kanigeuka nimemnyanyasia mwanaye. Nkajaribu kumweleza wala hakunielewa. Nikaamua kufungasafari, ile kufika tabu na polisi wanataka kunipeleka kituoni nikawakabidhi kwani Halima hajafika nyumbani.
Nikachanganyikiwa kabisa na nilipomkumbuka mwanagu kichaa kilizidi na hasira za kutosha. Niliamua kulala nyumba ya wageni sikupata usingizi wala sikulewa pombe.
Kesho yake niliondoka kurudi Moshi nikamweleza mama akanionea huruma akalia sana. Nikakagua chumba pesa zote kakomba, kuingia kwenye begi kachukua kila kinachomhusu. Nikatumia simu tofauti kumpigia akapokea kwa kuwa nilimtumia rafiki yake waliongea na mwisho akamtajia yupo porini Kikoletwa anajishughulisha na kilimo.
Na sasa ameolewa, pesa zimeisha anafanya vibarua mashambani kwa watu na mumewe ndipo wapate kula. Sijajua itakuwaje siku nikiwaona kwani nina hamu ya kuwaona.
Kitakachojiri nitakutumia kwani nimeshapajua napiga zoezi na pia nategemea kufanya miujiza na kuweka historia ya watakaobahatika kushuhudia siku hiyo. Nakutakia kazi njema dada yangu nami sitachoka kazi. (Kibadeni Limo mjukuu wa mboso. majanga)”.
Mpenzi msomaji, bila shaka umefuatilia kwa makini kisa hiki. Hakika kijana huyu ni jasiri na amejitahidi kwa kutumia mbinu zote lakini njiwa wake aliyempenda kapeperuka kama utani.
Lakini jambo la msingi alilofanya ni kule kumfuatilia hadi kufanikiwa sehemu aliko na ana hali gani. Bibie katoka kwenye boma analolelewa vema na kwa jeuri yake isiyo na mashiko anajikuta anaishia kulimishwa vibarua kwenye mashamba ya watu. Amekimbia kivulini akaishia juani. Au siyo msomaji wangu? Maisha Ndivyo Yalivyo.
Mpenzi msomaji, wapo kinamama ambao sijui ni madudu gani huwaingia akilini na kutifukatifuka hata kufikia kuchukua maamuzi yanayowapeleka kusiko. Angalia bibie huyo, kwa maelezo ya mumewe inaonyesha hakuwa na matatizo naye kwa maana ya matunzo kwani alifanya kila awezalo kuona maisha yao yanakuwa bora zaidi.
Angalia alimwachia bibie duka ili naye akaangalie kazi nyingine kuongeza kipato. Lakini hata pale alipopa kazi ile ambayo kwa maelezo ya kijana huyu ilimpa kipato kizuri, bibie hakumuelewa na badala yake kumfikiria vibaya kwamba eti huenda anaye hawara uko aendako.
Kazi ile ya kupeleka watalii Mlima Kilimanjaro siyo ya siku moja. Iliwachukua hadi wiki moja kabla ya kurudi nyumbani. Lakini mama pengine hakuweza kuyakubali mazingira ya kazi ya mumewe na ndiyo sababu wivu ukaanza kmtafuna. Kumbe alipaswa kuwa mtulivu na mvumilivu baada ya kumwelewa mumewe.
Sasa ametimka na kujikuta akiolewa na mtu mwingine ambaye ni mtafutaji kwa jasho jingi na kazi zenyewe za kuvizia vibarua vya kulima mashamba ya watu. Je, mazingira yaliyokuwa na nafuu ni yale ya kusimamia mauzo dukani au yale ya kuinama shambani kila kukicha na kusubiri ujira?
Kazi ni kazi sawa. Siyo kwamba nabeza kazi ile ya kulima la hasha! Lakini mama yule sidhani kama ana raha sana kwa mazingira yale ya sasa. Siyo ajabu anakumbuka maisha wakati akiwa na mume wa awali anajutia. Sitashangaa.

No comments:

Post a Comment