Thursday, 8 August 2013

Mwakyembe awatisha wavusha ‘unga’


WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataka watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kuachia ngazi endapo dawa za kulevya zitavushwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) bila wao kujua.
Dk. Mwakyembe alisema ni aibu na jambo la kushangaza kuona dawa zinavushwa wakati watendaji hao wapo, hivyo akawataka kujiwajibisha kwanza kabla ya hatua nyingine kufuata dhidi yao.
Waziri huyo alitoa tishio hilo jana wakati akizindua kamati ya nne ya kitaifa ya usalama wa usafiri wa anga, katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Dar es Salaam.
Mwakyembe ambaye aligoma kusoma hotuba yake aliyoandaliwa kwa ajili ya uzinduzi huo, alisisitiza kuwa endapo tukio kama hilo litatokea tena ni bora watendaji hao wakajiweka tayari kujiondoa mapema kabla hajawafikia.
Alisema hayo baada ya Mkurugenzi wa TCAA ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, Fadhil Manongi, kueleza kuwa ugaidi wa kimataifa unaendelea kuwa tishio kote duniani dhidi ya usalama wa maisha ya watu, mali zao na uchumi wa nchi.
Alisema suala la ulinzi na usalama katika viwanja vyetu ni fedheha na kashfa kubwa iliyoikumba nchi kutokana na kupitishwa kirahisi kwa dawa za kulevya kwenye JNIA, ambao unabeba jina la Baba yetu wa Taifa.
“Hivi ugaidi wa kitaifa ni nini? Kwa upande wangu dawa za kulevya ni sehemu yake. Mwenyekiti umetaka niielekeze hii kamati mpya, sidhani kama ilitakiwa kuelezwa kwa kuwa inajua wajibu wake.
“Tusitafute visingizio katika hili, huu ni udhaifu mkubwa ambao umetuletea ‘udhaifu’ mkubwa kitaifa,” alisema.
Mwakyembe aliongeza kuwa hali hiyo ya JNIA kuwa kituo cha dawa za kulevya, hadhani kama kunahitajika sheria zaidi kuhusu jambo hilo, badala yake akasisitiza kuwa: “Tumejidhalilisha, tunaonekana wote tuko kwenye mkumbo mmoja, hebu tufikie mahali tufanye wajibu wetu.”
Alisema kuwa amekuwa akisikia mjadala unaoendelea kuhusu dawa za kulevya, ambapo baadhi ya viongozi wanakataa kuheshimu sheria kwa kukwepe kukaguliwa.
Alisisitiza kuwa ni vema wakafuata taratibu kwani uwanja huo wa JNIA unadhalilika na kushuka hadhi kimataifa.
“Mimi nafikiri mnieleze nani anahusika. Hatuwezi kuendelea kujifanya viongozi wakati taifa linachafuka na tunaweza kuchukua hatua. Kama mtashindwa kuwataja nipeni majina hayo nitayataja mimi,” alisema.
Naye mjumbe wa kamati mpya, Balozi Irene Kasyanju, alisema kuwa wameliona tatizo la dawa za kulevya na wameshakaa na kuona namna gani ya kulitatua.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment