Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA ) uliopo jijini Dar es Salaam umevamiwa na ombaomba na kusababisha kero kwa abiria wa ndani na nje ya nchi wanaotumia uwanja huo.
Meneja Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, jana alimweleza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipotembelea uwanja huo kuwa ombaomba hao wameanza kujitokeza katika uwanja vya JNIA tangu wiki iliyopita na kujipenyeza sehemu wanayokaa abiria kabla ya kukaguliwa na kuwaomba fedha.
“Kuna mlemavu mmoja ndiyo msumbufu sana unamkuta amejipenyeza eneo la abiria na kuanza kuwaomba wazungu fedha, tumekuwa tukichukua jitihada za kuwaondoa lakini wanarudi,” alisema Jingu.
Ombaomba hao wakiwa wamejipanga pembeni mwa barabara ya kuingilia ndani ya uzio wa uwanja huo baadhi yao wakiwa na watoto wadogo na kila mtu anayepita karibu yao wanamuomba fedha.
Ombaomba hao baadhi wamekuwa wakitumia mbinu ya kutuma watoto wao wenye umri kati ya miaka 5 hadi 9 kuomba huku wazazi wao wakiwa wamekaa pembeni jambo ambalo limekuwa likishawishi abiria kulazimika kuwapatia pesa.
Kufuatia hali hiyo, Dk.Mwakyembe aliuagiza uongozi wa JNIA kufanya operesheni ya kuwaondoa ombaomba hao kwenye uwanja huo na kuweka udhibiti ambao utawafanya wasirejee tena.
Kumekuwa na ongezeko la ombaomba katika jiji la Dar es Salaam hususani wilaya ya Ilala na wengi wamekuwa wakibuni njia mbalimbali za kujipatia kipato, zikiwamo halali na zisizo halali.
chanzo;nipashe
No comments:
Post a Comment