STAA wa muziki aliyeachana na madawa ya kulevya, Rehema Chalamila ‘Ray C’, kwa mara ya kwanza ameibuka na kusimulia yaliyomkuta wakati akitumia madawa na kumfanya ashindwe kujitambua, Risasi Jumamosi linakujuza.
Akizungumza hivi karibuni kupitia Kipindi cha The Interview cha Clouds TV, mwanadada huyo alisema maisha hayo aliyafananisha na ya kuzimu kwani alikuwa hajitambui, alisukumwa kutenda mambo ya hovyo bila kujijua.
AELEZA HESHIMA YAKE
“Awali huko nyuma nilifaiti kujisomesha, kufanya kazi na kufanya biashara ambazo zilikuwa zikiniongezea kipato hadi kufikia hatua ya kujenga nyumba.
“Sijui ni shetani au ni nini? Ghafla nilijikuta naingia katika ulimwengu wa madawa ya kulevya na kuvuta bangi. Hata fedha nilizokuwa napata kwenye shoo na biashara zote ziliteketea,” alisema.
AMTAJA ALIYEMFUNDISHA
Katika mahojiano hayo, Ray C aliweka bayana kuwa chanzo cha yote ni baada ya kukutana na mpenzi wake (jina tunalo) ambaye ndiye aliyemfundisha kubwia unga na kuvuta bangi. Mwaka 2010 aliamua kuachana naye.
“Niliona ananipoteza, ilifika wakati hata muziki nikawa siwezi tena, nikawa nafanya kwa kujilazimisha, nikaamua kuachana naye,” alifunguka Ray C.
AISAKA SULUHU KENYA
Ray C alisema baada ya kuona ametopea kwenye madawa ya kulevya alitimkia nchini Kenya kwa ajili ya kujipanga tena akiamini ataweza kutafakari upya na kuacha kutumia unga.
Alisema alipofika nchini humo, hali haikubadilika.
AJUTA
Alisema: “Ulifika wakati, nikawa nalia mwenyewe hasa nilipokumbuka muda nilioupoteza kwa kufanya vitu ambayo nilikuwa sifikirii madhara yake.
“Nilijiuliza kwa nini nisirejee nyumbani kwa mama yangu ambaye naamini bado ananipenda?”
AREJEA BONGO
Baada ya kuishinda nguvu ambayo ilikuwa ikimsukuma kufanya maovu akiwa nchini Kenya, Ray C alisema aliamua kurudi Tanzania na kumueleza mama yake juu ya tatizo hilo la unga ambalo awali hakuwa amemuweka wazi.
Alisema licha ya kuamini kuwa alipotea, bado alijikuta akiendelea kutumia madawa hayo kwa kificho hata baada ya kupata msaada wa mama yake.
“Mama alihangaika sana. Alifanya maombi sana lakini sikuweza kurudi. Haikuwa akili yangu, sikuwa mimi, nilikuwa ulimwengu mwingine kabisa, sikuwa najielewa,” alisema.
GLOBAL YAMFICHUA
Novemba, mwaka jana Gazeti la Ijumaa la Global Publishers ndilo lilikuwa la kwanza kufichua hali ya Ray C baada ya kuandika habari iliyokuwa na kichwa kisemacho: DAH! RAY C na kuonesha picha ambazo mwanadada huyo alivyoathirika na madawa ya kulevya.
Baada ya gazeti hilo kuingia mtaani, walijitokeza wadau mbalimbali kumsaidia, akiwemo Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ‘JK’ na Kampuni ya Clouds Media Group ambao walimpa msaada wa kitaalamu wa kumpeleka kwenye kitengo maalum cha madawa ya kulevya kilichopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar.
AANZA TIBA
“Nilipewa msaada pale kitengo maalum cha madawa ya kulevya Muhimbili. Walinitibu kisaikolojia, nikahudhuria kliniki kwa miezi tisa na ninaendelea vizuri,” alisema Ray C.
chanzo:.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment